Kharrazi: Iran iko tayari kwa mazungumzo, lakini haitakubali kuburuzwa
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni ya Iran, Kamal Kharrazi amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kwa mazungumzo, lakini katu haitakubali kutwishwa matakwa ya aina yoyote.
Dakta Kharrazi ameyasema hayo katika mahojiano na tovuti rasmi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei (khamenei.ir) yaliyochapishwa Jumatano.
Afisa huyo mwandamizi wa Iran ameashiria kanuni tatu kuu ambazo zimeelezwa na Kiongozi Muadhamu kama msingi wa mchakato wowote wa mazungumzo yenye staha na unaostahiki ushiriki wa Jamhuri ya Kiislamu; ambazo ni utu, hekima na ustahiki.
"Iwapo mazungumzo yatafanyika kwa misingi ya mantiki na hadhi ya Jamhuri ya Kiislamu ikiheshimiwa, tuko tayari kuzungumza, madhali tu tusitwishwe chochote. Iwapo kutakuwa na jaribio lolote la kulazimishwa na kuburuzwa, tutasimama dhidi yake," amebainisha.
Kharrazi, ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema "Suluhisho pekee la changamoto za Asia Magharibi ni mazungumzo ya moja kwa moja kati ya nchi za eneo hilo bila ya uingiliaji wa madola ya nje ya kanda hii."
Kharrazi akirejelea matamshi yaliyotolewa na Kiongozi Muadhamu mwezi uliopita, ambapo Ayatullah Khamenei alipinga matakwa ya Marekani kuhusu mazungumzo ya nyuklia, amesema kwamba kukubali mazungumzo chini ya vitisho ni jambo ambalo "hakuna taifa linalojiheshiku linaweza kufanya, na hakuna mwanasiasa mwenye busara angeweza kuidhinisha."
Kwingineko katika matamshi yake, Kharrazi amezungumzia shutuma zisizokwisha za nchi za Magharibi dhidi ya Iran za "kugengeuka" mpango wake wa nyuklia. Amesema, "Wamagharibi hawachukulii fatwa ya kuharamisha silaha za nyuklia kwa uzito, kwa sababu hawana uelewa wa utamaduni wetu wa kidini, na wanadhani Iran inaweza kubadilisha mkondo (w mradi huo) katika siku zijazo."