Angola yatangaza kuwekeza kwenye satelaiti mpya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132582-angola_yatangaza_kuwekeza_kwenye_satelaiti_mpya
Serikali ya Angola imetangaza kuwa itaongeza uwekezaji katika sekta ya mawasiliano ya simu, ambao utajumuisha mpango wa kurusha satelaiti mpya ya uchunguzi na kupanua mtandao wa taifa wa mawasiliano kama sehemu ya mkakati mpana wa kufaidika vizuri na teknolojia za kisasa zinazojumuisha watu wote nchini humo.
(last modified 2025-10-30T06:46:16+00:00 )
Oct 30, 2025 06:46 UTC
  • Angola yatangaza kuwekeza kwenye satelaiti mpya

Serikali ya Angola imetangaza kuwa itaongeza uwekezaji katika sekta ya mawasiliano ya simu, ambao utajumuisha mpango wa kurusha satelaiti mpya ya uchunguzi na kupanua mtandao wa taifa wa mawasiliano kama sehemu ya mkakati mpana wa kufaidika vizuri na teknolojia za kisasa zinazojumuisha watu wote nchini humo.

Rais Joao Lourenco wa Angola ametangaza mkakati huo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Ufadhili wa Maendeleo ya Miundombinu ya Afrika uliofanyika katika mji mkuu nchi hiyo, Luanda.

Rais Lourenco amesema kuwa, serikali ya Angola imejitolea kuhakikisha kunakuwa na fursa sawa za matumizi ya teknolojia za kidijitali na kutumia uvumbuzi wa kiteknolojia kwaajili ya maendeleo ya taifa.

Rais Joao Lourenco wa Angola

 

Amesema: "Katika mawasiliano ya simu, tunawekeza kwenye satelaiti nyingine ya uchunguzi wa Dunia na kupanua mtandao wa taifa wa mawasiliano kote nchini ili kuleta suluhisho la kidijitali na uvumbuzi wa kiteknolojia kwa wananchi wote wa Angola.

Angola ilizindua satelaiti yake ya kwanza ya taifa ya mawasiliano ya simu inayoitwa Angosat-2, mwezi Oktoba 2022. Satelaiti hiyo inatoa huduma katika sehemu zote za Angola na sehemu kubwa ya Afrika, ikiboresha upatikanaji wa intaneti, huduma za utangazaji na mawasiliano ya data.

Serikali ya Angola imesema pia kuw, inawekeza katika miradi muhimu ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ambayo ni nguzo ya kimkakati ya ustawi mseto wa kiuchumi na ujumuishaji wa kikanda. Hayo yamo kwenye Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063.