Wasudan 177,000 wamekwama katika mji ulioteketea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132728-wasudan_177_000_wamekwama_katika_mji_ulioteketea
Mji wa El Fasher, ambao ni makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan, hatimaye ulitekwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF hivi karibuni baada ya kuzingirwa kwa muda wa miezi 18 na hivi sasa ripoti zinasema kuwa Wasudan 177,000 wamekwama kwenye mji huo.
(last modified 2025-11-03T05:42:54+00:00 )
Nov 03, 2025 02:23 UTC
  • Wakimbizi wa Sudan, El Fasher
    Wakimbizi wa Sudan, El Fasher

Mji wa El Fasher, ambao ni makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan, hatimaye ulitekwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF hivi karibuni baada ya kuzingirwa kwa muda wa miezi 18 na hivi sasa ripoti zinasema kuwa Wasudan 177,000 wamekwama kwenye mji huo.

Baada ya kutekwa mji wa El-Fasher, hivi sasa nchi ya Sudan ni kama vile imegawika vipande viwili, kimoja ni cha utawala wa mashariki chini ya udhibiti wa jeshi SAF na kingine ni cha magharibi chini ya udhibiti wa Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF. Kinacholeta mguso zaidi ni kwamba mji wa El Fasher haukutoka mikononi mwa SAF kwa nguvu za ndani tu za waasi, bali kuna mikono ya nje ya Sudan imehusika moja kwa moja kwenye kutekwa mji huo na kundi la RSF.

Mapigano ya silaha nchini Sudan yalianza Aprili 15, 2023 kutokana na uchu wa madaraka kati ya majenerali wa kijeshi. Baadhi ya majenerali hao wanaongoza SAF chini ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kundi la pili ni lile la Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF chini ya Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la Hemedti.

Vita hivyo vya uchu wa madaraka baina ya majenerali hao wa kijeshi vilizuka baada ya Jenerali Al Burhan kutaka Vikosi vya Msaada wa Haraka viwekwe chini ya jeshi la Sudan kufuati mapinduzi ya 2021 na RSF wakakataa. Hadi sasa kumeshafanyika upatanishi mwingi wa kimataifa lakini umeshindwa kutatua mgogoro wa Sudan.

Katika siku za hivi karibuni na baada ya kutekwa mji wa El Fasher, watawala wa Khartoum, Umoja wa Mataifa na taasisi na mashirika mengine ya kimataifa yamekuwa yakiishutumu RSF kwa kufanya "mauaji ya umati na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia wa mji huo.