UN yalaani shambulio lililoua askari 6 wa kulinda amani Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134276-un_yalaani_shambulio_lililoua_askari_6_wa_kulinda_amani_sudan
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa na shambulio la ndege isiyo na rubani lililolenga kituo cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan, na kuwaua askari sita wa kulinda amani wa umoja huo.
(last modified 2025-12-14T02:36:10+00:00 )
Dec 14, 2025 02:36 UTC
  • UN yalaani shambulio lililoua askari 6 wa kulinda amani Sudan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa na shambulio la ndege isiyo na rubani lililolenga kituo cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan, na kuwaua askari sita wa kulinda amani wa umoja huo.

Guterres amesema katika taarifa yake kwamba, shambulio hilo la jana Jumamosi lililenga kambi lojistikki ya askari hao wa kulinda amani katika mji wa Kadugli, katika eneo la kati la Kordofan.

Walinda amani wengine wanane wamejeruhiwa katika hujuma hiyo. Wahanga wote wa shambulio hilo ni raia wa Bangladesh, waliokuwa wakihudumu katika Kikosi cha Mpito cha Usalama cha Umoja wa Mataifa cha Abyei (UNISFA).

"Ninalaani vikali mashambulizi ya kutisha ya ndege zisizo na rubani yaliyolenga kambi ya lojistiki ya walinda amani ya Umoja wa Mataifa huko Kadugli, Sudan," Guterres amesema katika taarifa.

Haya yanajiri siku moja baada ya shambulio jingine la droni kuua raia wasiopungua 30 katika Jimbo la Darfur Kusini, huko Sudan. Shambulio hilo liliripotiwa kutokea katika eneo lililoko takriban kilomita 150 kusini-magharibi mwa makao makuu ya jimbo hilo yaani mji wa Nyala. 

Katibu Mkuu wa UN amekariri mwito wake kwa mataifa yote yenye ushawishi kwa pande mbili zinazopigana huko Sudan, kuzilazimisha zisimamishe vita mara moja na zizuie kumiminwa silaha huko Sudan.

Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF na Jeshi la Sudan SAF vilianza kupigana tarehe 15 Aprili 2023 kutokana na uchu wa madaraka. Mgogoro wa Sudan umeshapelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuhama makazi yao. Sudan hivi sasa inashuhudia moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.