Umoja wa Mataifa: Zaidi ya wakimbizi 50 wa Congo wamefariki Burundi
-
Umoja wa Mataifa: Zaidi ya wakimbizi 50 wa Congo wamefariki Burundi
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya wakimbizi 50 wanaokimbia mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamefariki duniani katika nchi jirani ya Burundi.
Hayo yameelezwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).
Taarifa ya UNHCR imeeleza kuwa, kati ya jumla ya vifo 53 vilivyorekodiwa, watu 25 walikufa kutokana na mlipuko wa kipindupindu, huku wengine sita wakifariki dunia kutokana na upungufu wa damu na matatizo mengine yanayohusiana na utapiamlo.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, unashirikiana na wizara ya afya na washirika wengine kuchunguza chanzo cha vifo vingine.
Zaidi ya Wacongo 100,000 wametafuta hifadhi katika nchi jirani ya Burundi tangu mapigano karibu na mpaka yalipozidi mapema Desemba mwaka jana (2025) na waasi kuuteka mji wa Uvira, UNHCR ilisema.
Jean Jacques Purusi, gavana wa jimbo la Kivu Kusini ambapo Uvira iko, alielezea hali nchini Burundi kama "matatizo" na "mgogoro uliosahaulika kabisa na jamii ya kimataifa na vyombo vya habari."
Wizara ya mambo ya ndani na kijamii ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilisema inaongoza misheni ya kibinadamu kuwasaidia Wacongo waliokimbia makazi yao nchini Burundi, kwa kutoa chakula, dawa, na vitu visivyo vya chakula.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mapigano makali yaliibuka wiki iliyopita kati ya waasi wenye silaha wa kundi la M23 na vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya Kinshasa katika miji kadhaa karibu na mji wa Uvira, mashariki mwa DR Congo, vyanzo vya ndani vilisema.
Eneo lenye utajiri mkubwa wa maliasili la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambalo linapakana na Rwanda na Burundi limekumbwa na mchafuko yanayoendelea kwa miaka 30 sasa.