Afrika Kusini yatetea mazoezi ya kijeshi ya BRICS
Serikali ya Afrika Kusini imetetea mazoezi ya kijeshi ya wiki moja yanayozishirikisha nchi kubwa za Russia, Iran, China na nchi nyingine muhimu, ikisema kuwa maneva hayo kwenye pwani yake ni majibu muhimu ya kuzuia kuongezeka mivutano ya baharini ulimwenguni.
Luteka hiyo ya kijeshi iliyopewa jina la "Will for Peace 2026" iliyoanza jana Jumamosi katika fukwe za Cape Town yanafanyika siku chache baada ya Marekani kuteka meli ya mafuta ya Russia katika bahari ya Atlantiki ya Kaskazini, ikidai kuwa imekiuka vikwazo vya madola ya Magharibi.
Mazoezi hayo ya majini pia yamekuja wakati ambapo mvutano umeongezeka kati ya utawala wa Donald Trump huko Marekani na nchi kadhaa za "BRICS Plus," zikiwemo China, Iran, Afrika Kusini na Brazil.
Kapteni Nndwakhulu Thomas Thamaha, kamanda wa kikosi kazi cha pamoja cha Afrika Kusini, ameiambia hafla ya ufunguzi wa mazoezi hayo ya jana Jumamosi kwamba luteka hiyo ni zaidi ya mazoezi ya kijeshi na ni zaidi ya taarifa ya BRICS.
BRICS ambayo asili yake iliundwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini imepanuka na kuzijumuisha nchi za Misri, Ethiopia, Iran, Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu na Indonesia.
China na Iran zilipeleka meli zake kubwa za kivita huko Afrika Kusini, huku Russia na Muungano wa Falme za Kiarabu nazo zimetuma meli zao huko Afrika Kusini. Nchi za Indonesia, Ethiopia na Brazil nazo zimejiunga kwenye mazoezi hayo ya kijeshi kama waangalizi.
Naibu Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Bantu Holomisa alisema Ijumaa kwamba mazoezi hayo yalipangwa kufanyika muda mrefu nyuma kabla ya kuongezeka mvutano wa kimataifa.