OIC imefanya kikao kujadili kadhia ya Somaliland, baada ya Wazayuni kuitambua rasmi
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imeitisha kikao mjini Jeddah, Saudi Arabia kujadili kadhia ya Somaliland na hasa baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutambua rasmi kujitenga na ardhi nyingine za Somalia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, kikao hicho cha dharura cha OIC kimejikita zaidi katika kujadili njama kubwa za utawala wa Kizayuni za kuzigawa nchi za Waislamu kupitia kuitambua rasmi Somaliland kuwa nchi huru.
Kikao hicho kimefanyika siku chache baada ya nchi 22 za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kutoa taarifa na kutangaza kuwa zinapinga vikali kujitenga eneo la Somaliland na ardhi nyingine ya Somalia sambamba na kulaani vikali safari ya waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hilo.
Taarifa hiyo ilisema: "Tunalaani safari iliyo kinyume cha sheria ya afisa mwandamizi wa utawala wa Kizayuni katika eneo la Somaliland ambalo ni sehemu ya ardhi ya Somalia. Safari hiyo imekiuka mamlaka ya kujitawala Somalia na ni kinyume cha Hati ya Umoja wa Mataifa."
Nchi za bara Afrika, za Kiarabu na za Kiislamu zinahofia kwamba, uwepo wa Israel katika Pembe ya Afrika kupitia Somaliland ni jambo ambalo litavuruga mlingano wa kiusalama katika Bahari Nyekundu na kugeuza eneo hilo kuwa uwanja wa makabiliano ya moja kwa moja na ya gharama kubwa.
Kikao hicho kimefanyika huku Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Ahmed Moalim Fiqi, akiilaumu vikali Israel kwa kupanga kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza na kuwapeleka Somaliland, akiulaani mpango huo alioutaja kuwa ni "ukiukaji mkubwa" wa sheria za kimataifa.
Katika mahojiano na Televisheni ya Al Jazeera jana Jumamosi, Waziri Fiqi alietoa mwito kwa Benjamin Netanyahu afutilie mbali tangazo lake la kuitambua Somaliland, akiieleza hatua hiyo kuwa ni "hujuma ya moja kwa moja" dhidi ya haki ya kujitawala Somalia.