Kwa nini Misri inapinga kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina hadi Somaliland?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135414-kwa_nini_misri_inapinga_kuhamishwa_kwa_nguvu_wapalestina_hadi_somaliland
Misri imetangaza kupinga vikali kuhamishwa kwa lazima kwa Wapalestina hadi Somaliland eneo lililotangaza kujitenga na Somalia.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 13, 2026 00:10 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdel Ati
    Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdel Ati

Misri imetangaza kupinga vikali kuhamishwa kwa lazima kwa Wapalestina hadi Somaliland eneo lililotangaza kujitenga na Somalia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdel Ati alisisitiza upinzani wake dhidi ya kulazimishwa kwa Wapalestina kuhamishwa hadi Somaliland na utawala wa Kizayuni.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Afrika uliofanyika kwa njia ya mawasiliano ya Intanet, alisema kwamba kitendo cha upande mmoja cha Israel kutambua eneo la "Somaliland" ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala, uhuru, na umoja wa ardhi wa Jamhuri ya Somalia na ukiukaji wa sheria za kimataifa, mkataba wa Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Umoja wa Afrika. Aliongeza: "Kitendo hiki cha Israel ni hatari na tishio kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa, ambacho kinahitaji msimamo mmoja wa kuunga mkono Somalia na juhudi za pamoja za kufikia usalama na utulivu katika nchi hiyo na eneo la Pembe ya Afrika."

Kuhusiana na suala hili, nchi 22 na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) zililaani vikali hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuitambua Somaliland katika taarifa ya pamoja. Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia zimetangaza kupinga kwao hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuitambua "Somaliland" kama eneo linalojitawala.

Abdel Ati pia alisisitiza kwamba ukimya kuhusu vitendo hivi vya upande mmoja, vinavyotishia utulivu wa bara la Afrika, hauruhusiwi, na kwamba vitendo hivi vinalenga kulazimisha hali mpya za kisiasa nje ya mfumo wowote wa kisheria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri pia alisisitiza uungaji mkono kamili wa nchi yake kwa mamlaka ya kujitawala, uhuru, na umoja wa ardhi ya Somalia, akiitaja kuwa nguzo ya msingi kwa utulivu wa Pembe ya Afrika na eneo la Bahari Nyekundu. Alieleza kwamba hatua hii ya Israel itasababisha kuongezeka kwa migogoro na ukosefu wa usalama katika eneo hilo, na kuhusisha matokeo kamili ya uamuzi huu haramu na utawala wa Kizayuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri pia alisisitiza upinzani wake mkali kwa jaribio lolote la kuunganisha hatua hii haramu na mipango ya kuwaondoa kwa nguvu watu wa Palestina kutoka katika ardhi yao, akisema kwamba vitendo hivyo havikubaliki na ni kinyume cha sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na Mkataba wa Umoja wa Afrika.

Msimamo mkali na wazi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri dhidi ya uhamisho wa Wapalestina hadi Somaliland uliambatana na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Sa'ar hadi Hargeisa, mji mkuu wa eneo linalojiendesha la Somaliland. Wiki tatu zilizopita, Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu alitambua eneo hilo kama nchi huru inayojitawala, kitendo haramu kilichokiuka uhuru wa Somalia,  na ambacho kiliibua hasira kubwa kutoka kwa nchi mbalimbali na serikali kuu ya Somalia.

Misri imepinga kimkakati na kwa uthabiti mpango wowote wa kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu hadi Somaliland. Msimamo huu hautegemei tu kanuni za sera za kigeni zilizowekwa na Cairo, lakini pia ulionyeshwa moja kwa moja katika taarifa za Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri katika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na Baraza la Amani na Usalama la Afrika. Misri imeonya kwamba Israel inajaribu kutumia kuitambua rasmi Somaliland kwa  upande mmoja ili kuendeleza "mipango haramu" inayohusiana na kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu.

Sababu ya kwanza ya upinzani wa Misri ni dai la kutetea haki za kihistoria na kisheria za watu wa Palestina. Cairo imesisitiza kwamba mpango wowote wa kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na jaribio la kuondoa suala la Palestina kupitia kufuta kizazi na kaumu. Misri imesema kwamba kutumia kesi ya Somaliland kuendeleza mipango kama hiyo ni jambo ambalo "halikubaliki kabisa" na ni kinyume cha kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Sababu ya pili ni wasiwasi kwamba Israel itatumia vibaya hali ya Somaliland. Israel iliitambua Somaliland mnamo Desemba 2025, hatua ambayo Misri iliielezea kama "tishio kubwa kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa." Cairo ilionya kwamba utambuzi huo unaweza kusababisha kuundwa kwa hali isiyo  halisi ya kisiasa na kusafisha njia ya mipango ya kulazimishwa kuhama kwa Wapalestina.

Sababu ya tatu ni ulinzi wa Misri kwa umoja wa ardhi wa Somalia. Cairo imerudia kusema kwamba Somaliland ni sehemu ya Somalia na kwamba kuitambua itakuwa ni ukiukaji wa uhuru wake. Misri imesisitiza kwamba matumizi yoyote ya eneo hili kwa ajili ya makazi ya Wapalestina kwa lazima yatakuwa ni ukiukaji maradufu wa sheria za kimataifa na tishio kwa utulivu wa Pembe ya Afrika.

Sababu ya nne ni wasiwasi kuhusu usalama na athari za kikanda. Misri inaamini kwamba kulazimishwa kwa Wapalestina kutawanywa sio tu kwamba kutasababisha mgogoro wa kibinadamu, lakini pia kunaweza kuibua wimbi la ukosefu wa utulivu katika Asia Magharibi na Afrika. Cairo imeonya kwamba mipango kama hiyo itazidisha mgawanyiko na hitilafu kuhusu Gaza na kuuandaa mazingira ya mzozo mpana zaidi.

Misri pia inaona mipango hii kama sehemu ya njama za kufuta haki ya Wapalestina kurejea katika ardhi za asili. Cairo imesisitiza kwamba hakuna nchi inayopaswa kuruhusu Israel kugeuza suala la Palestina kutoka katika mkondo wake wa kisheria kwa kuunda migogoro bandia. Kwa hivyo, upinzani wa Misri dhidi ya kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina hadi Somaliland ni mchanganyiko wa masuala ya kisheria, kibinadamu, usalama, na kijiografia ambayo yamesemwa wazi katika misimamo rasmi ya nchi hiyo.