RSF yaua watu 27 huko Sennar, mashariki mwa Sudan
-
Sennar, Sudan
Watu 27 wameuawa na wengine 13 kujeruhiwa katika shambulio la wapiganaji wa Rapid Support Forces lililolenga mji wa Sinja, wakati watu waliokimbia makazi yao kutoka Darfur Kaskazini wakiendelea kuongezeka, huku Jeshi la Sudan likitangaza mauaji ya mamia ya wanachama wa RSF katika maeneo tofauti.
Chanzo cha jeshi la Sudan kimesema kwamba wapiganaji wa RSF wameshambulia mji wa Sinja, katika Jimbo la Sennar kusini-mashariki mwa nchi, kwa kutumia ndege isiyo na rubani. Ameongeza kuwa mabomu hayo yalilenga timu za usalama na baadhi ya raia waliokuwa wakiandamana na viongozi wa jeshi kutoka majimbo kadhaa.
Msemaji rasmi wa serikali ya Sennar, Salah Adam Abdullah, amesema kwamba "ndege ya kimkakati isiyo na rubani ililenga mji wa Sinja jana Jumatatu, na kwamba mashambulizi hayo yamesababisha hasara na majeraha miongoni mwa raia.
Ripoti zinasema, Gavana wa Jimbo la White Nile, Qamar al-Din Fadl al-Mawla, amenusurika shambulio dhidi ya mji wa Sinja, ambapo alikuwa akihudhuria mkutano rasmi, lakini wenzake wawili wameuawa katika shambulio hilo.
Shambulizi hilo limefanyika siku moja baada ya serikali ya Sudan kutangaza kurejea kwake katika mji mkuu, Khartoum, baada ya karibu miaka mitatu ya kuhamia Port Sudan.