Somalia yafuta mikataba yote iliyosainiwa na UAE
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135430-somalia_yafuta_mikataba_yote_iliyosainiwa_na_uae
Somalia imeamua kufuta makubaliano yote yaliyosainiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu, ili kukabiliana na hatua za Abu Dhabi zinazodhoofisha mamlaka, umoja na uhuru wa nchi hiyo. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la Mawaziri la Somalia.
(last modified 2026-01-13T02:33:12+00:00 )
Jan 13, 2026 02:33 UTC
  • Bandari ya Somalia
    Bandari ya Somalia

Somalia imeamua kufuta makubaliano yote yaliyosainiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu, ili kukabiliana na hatua za Abu Dhabi zinazodhoofisha mamlaka, umoja na uhuru wa nchi hiyo. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la Mawaziri la Somalia.

Taarifa hiyo imefafanua kwamba Baraza la Mawaziri limesitisha makubaliano yote na Serikali ya Falme za Kiarabu, ikiwa ni pamoja na mashirika ya serikali, vyombo vyenye uhusiano na idara za kikanda ndani ya nchi.

Taarifa hiyo imesema kwamba uamuzi huu unajumuisha makubaliano yote yaliyopo na ushirikiano katika bandari za Berbera, Bosaso na Kismayo.

Imeongeza kuwa kufutwa kwa makubaliano yote na UAE, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya usalama na ulinzi, kunakuja "kutokana na ripoti na ushahidi madhubuti unaohusiana na hatua hasi zinazoathiri mamlaka ya nchi, umoja wa kitaifa na uhuru wa kisiasa."

Somalia imesisitiza kwamba vitendo hivyo vinakiuka kanuni za mamlaka ya kujitawala, kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, na udharura wa kuheshimu utaratibu wa kikatiba wa serikali.

Mkataba wa usalama uliosainiwa kati ya nchi hizo mbili, ambao ulilenga ushirikiano wa kijeshi na kupambana na ugaidi, ulieleza kwamba UAE itatoa msaada kwa vikosi vya jeshi la Somalia kupitia mafunzo na misaada ya silaha, pamoja na kuiruhusu kutekeleza operesheni za kijeshi na kiusalama ndani ya ardhi ya Somalia kwa njia ya nchi kavu, baharini, na angani.

Pia yalijumuisha vifungu vinavyoiruhusu UAE kutumia bandari na viwanja vya ndege vya Somalia, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vya kijeshi.