Somalia yaitaka Israel kubatilisha mara moja uamuzi wake wa kuitambua Somaliland
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135454-somalia_yaitaka_israel_kubatilisha_mara_moja_uamuzi_wake_wa_kuitambua_somaliland
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia ameitaja hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kulitambua eneo la Somaliland kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya nchi yake.
(last modified 2026-01-13T23:10:09+00:00 )
Jan 13, 2026 23:10 UTC
  • Somalia: Israel ibatilishe kuitambua Somaliland
    Somalia: Israel ibatilishe kuitambua Somaliland

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia ameitaja hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kulitambua eneo la Somaliland kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya nchi yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Abdisalam Abdi Ali ametangaza katika taarifa kwamba, uhuru na umoja wa ardhi ya nchi umehifadhiwa kikamilifu na hautishiwi na tishio lolote.

Aliongeza: "Uhuru na umoja wa eneo la Somalia hauwezi kujadiliwa, kulingana na katiba, maazimio ya bunge na misimamo ya rais."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia alisisitiza kwamba, hatua ya Israel ya kulitambua eneo la Somalia la Somaliland kuwa huru na lenye mamlaka ni kinyume cha sheria na ni ukiukaji dhahiri wa uhuru wa Somalia, na uamuzi huu lazima ufutwe mara moja.

Aliongeza: "Serikali ya Somalia itatumia njia zote za kidiplomasia na kisheria kutetea uhuru wake na umoja wa ardhi yake."

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Ahmed Moalim Fiqi, ameishutumu Israel kwa kupanga kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kuwapeleka katika eneo lililojitenga la Somaliland, akiukashifu mpango huo alioutaja kuwa ni "ukiukaji mkubwa" wa sheria za kimataifa.

Haya yanajiri siku chache baada ya nchi 22 za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kutoa taarifa na kutangaza kuwa zinapinga vikali kujitenga eneo la Somaliland la Somalia sanjari na kulaani vikali safari ya waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hilo.