Uganda: Serikali yazima mtandao wa intaneti siku moja kabla ya uchaguzi mkuu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135476-uganda_serikali_yazima_mtandao_wa_intaneti_siku_moja_kabla_ya_uchaguzi_mkuu
Serikali ya Uganda imezima mtandao wa intaneti siku moja kabla ya kuelekea uchaguzi mkuu wa hapo kesho, uchaguzi ambao Rais Yoweri Museveni anataka kuchaguliwa kwa muhula wa saba.
(last modified 2026-01-14T07:24:23+00:00 )
Jan 14, 2026 07:24 UTC
  • Uganda: Serikali yazima mtandao wa intaneti siku moja kabla ya uchaguzi mkuu
    Uganda: Serikali yazima mtandao wa intaneti siku moja kabla ya uchaguzi mkuu

Serikali ya Uganda imezima mtandao wa intaneti siku moja kabla ya kuelekea uchaguzi mkuu wa hapo kesho, uchaguzi ambao Rais Yoweri Museveni anataka kuchaguliwa kwa muhula wa saba.

Mamlaka ya mawasiliano katika taifa hilo la Afrika Mashariki inasema imechukua hatua hiyo kuzuia usambazwaji wa habari za kupotosha na kuchochea vurugu.

Licha ya kuthibitisha kuzima intaneti, haikuweka wazi ni lini huduma hiyo itarejeshwa au makataa hayo yatadumu kwa muda gani, jambo ambalo tayari limeibua maswali kuhusu uwazi kuelekea uchaguzi wa hapo kesho.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya ndani na nje ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki yameonya dhidi ya hatua hii, waliyosema ni wazi ina nia ovu kutaka kuwaweka raia gizani ili wasipate taarifa kwa wakati.

Hatua hii ya mamlaka ya mawasiliano imekuja juma moja kupita tangu mkurugenzi wake akanushe taarifa kuwa serikali ilikuwa na mpango wa kuzima intaneti kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Hatua sawa na hii ilichukuliwa pia katika uchaguzi wa mwaka wa 2021, uchaguzi ambao hata hivyo uligubikwa na udaganyifu pamoja na mamlaka kutumia nguvu dhidi ya wapinzani.

Uchaguzi mkuu wa Uganda umepangwa kufanyika Januari 15, 2026 kumchagua rais, bunge, na serikali za manispaa. Kuna mchanganyiko wa matumaini, hofu na mashaka kuhusu mustakabali wa demokrasia na utawala nchini humo.

Akiwa na umri wa miaka 81, Museveni anawania kuchaguliwa tena akibeba bendera ya chama tawala cha National Resistance Movement, NRM baada ya kuweko madarakani kwa karibu miaka 40.

Mshindani wake mkuu Bobi Wine amejenga matumaini ya mabadiliko nchini humo. Mwimbaji huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita wa urais mnamo 2021, kwa kupata 35% ya kura. Wine alidai ushindi wake uliibwa kupitia ujazo wa kura na makosa mengine. Hata hivyo tume ya uchaguzi wa Uganda ilikanusha madai hayo.