Indhari ya Hamas kuhusu hali mbaya ya kibinadamu Gaza
-
Indhari ya Hamas kuhusu hali mbaya ya kibinadamu Gaza
Baada ya kufariki kwa idadi ya watoto wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza kutokana na baridi kali, Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombzoi wa Palestina, Hamas, imeonya kuhusu kuzidi kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika eneo hilo ambalo liko chini ya mzingiro wa utawala katili wa Israel.
Kwa mujibu wa ripoti ya Al-Alam, katika taarifa yake, Hamas imesema kuna ukosefu wa vifaa muhimu vya kuwalinda wakazi dhidi ya baridi kali katika kambi za wakimbizi za Gaza,
Aidha Hamas imesema kuwa Wapalestina zaidi wanapoteza maisha kila siku katika Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya utawala wa Israel, kuporomoka kwa majengo yaliyoharibiwa nusu, hali mbaya ya hewa, na hatua ya utawala huo kuzuia kuingia kwa misaada ya kibinadamu inayohitajika kwa dharura.
Hamas imezitaka pande zinazojaribu kusuluhisha mgogoro huo zitoe shinikizo kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ili usitishe vizuizi vinavyokwamisha kuwasili kwa misaada Gaza.
Katika kipindi cha siku mbili zilizopita, Gaza imekumbwa na maafa makubwa baada ya Wapalestina 24 kupoteza maisha kutokana na mvua kubwa, kuporomoka kwa nyumba, na kuharibiwa kwa idadi kubwa ya mahema, kwa mujibu wa ofisi ya habari ya serikali ya Gaza.
UNICEF pia imeripoti kuwa zaidi ya watoto 100 wa Kipalestina wameuawa Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano kuanze, baadhi yao wakidaiwa kuuawa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Israel.
Utawala wa Israel ulianzisha kampeni yake ya kijeshi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 2023, na kuua zaidi ya Wapalestina 70,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Uvamizi wa Israel dhidi ya Gaza, unaoungwa mkono na Marekani, pia umesababisha uharibifu mkubwa, huku takribani asilimia 90 ya miundombinu ya Ukanda huo ikiharibiwa.