Wananchi wa Uganda wanapiga kura leo, Museveni atarajiwa kuendelea kutawala
-
Wananchi wa Uganda wanapiga kura leo, Museveni atarajiwa kuendelea kutawala
Wananchi wa Uganda waliotimiza masharti ya kupiga kura, leo wanaelekea katika vituo vya kupigia kura kuamua hatiam ya uongozi wa nchi hiyo kwa miaka mingine mitano.
Raia zaidi ya milioni 21 wa Uganda wanapiga kura leo katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kuendeleza utawala wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni.
Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa moja asubuhi na vitafungwa saa kumi alasiri kwa saa za Afrika Mashariki, huku mshindi akitarajiwa kutangazwa ifikapo Jumamosi mchana.
Museveni mwenye umri wa miaka 81 na aliye madarakani tangu mwaka 1986, anawania muhula wa saba, huku kukiwa na hofu kuhusu uwazi wa mchakato huo hasa wakati huu kukiwa kumezimwa mtandao wa intaneti na mawasiliano.
Hata hivyo, Museveni anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 43, anayewakilisha kizazi kinachotamani mabadiliko ya kisiasa katika taifa la Afrika Mashariki lenye watu takribani milioni 45.
Wakati Uganda ikiingia kwenye uchaguzi wa rais, hatua za kuzima mtandao, kuwepo kwa wanajeshi mitaani na madai ya kuingiliwa kwa mchakato zimeibua maswali mazito kuhusu uwazi wa kura na mustakabali wa demokrasia.
Mshindani wake mkuu Bobi Wine amejenga matumaini ya mabadiliko nchini humo. Mwimbaji huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita wa urais mnamo 2021, kwa kupata 35% ya kura. Wine alidai ushindi wake uliibwa kupitia ujazo wa kura na makosa mengine. Hata hivyo tume ya uchaguzi wa Uganda ilikanusha madai hayo.