ANC yaonya kuhusu njama za 'mapinduzi' nchini Iran
-
Chma cha ANC
Mkuu wa vuguvugu la Mshikamano wa Kimataifa wa chama tawala cha African National Congress (ANC) katika jimbo la Western Cape nchini Afrika Kusini ameonya kwamba, machafuko ya hivi karibuni nchini Iran yana mkono wa Marekani na washirika wake wa Kizayuni.
Khalid Sayed, katika mahojiano na shirika la habari la Iran Press amesema, "Taarifa zinazotoka Washington na kutoka kwa maafisa wa Kizayuni zinaashiria waziwazi kuwepo majaribio ya kuupindua mfumo wa kisiasa wa Iran."
Ameeleza bayana kuwa, "Baada ya uingiliaji kati haramu wa Marekani nchini Venezuela na kutekwa nyara kwa rais wa nchi hiyo (Nicolas Maduro), nchi za dunia zina haki ya kuuliza: ni nani anayefuata?"
Sayed amesema, "Eneo la Kusini mwa Dunia linahitaji kuungana na kuchukua msimamo wa pamoja dhidi ya vitisho vinavyotolewa na Marekani na washirika wake."
Mkuu wa Mshikamano wa Kimataifa wa chama tawala nchini Afrika Kusini amebainisha kuwa, "Vikwazo vilivyowekwa na Magharibi dhidi ya Iran vimeleta ugumu wa kiuchumi unaoathiri wafanyakazi zaidi. Vikwazo hivi havina mfungamano na haki za binadamu, bali ni chombo cha kuburuzana."
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa ANC ameongeza, "Huku Rais Donald Trump akitangaza ushuru wa asilimia 25 kwa nchi zinazofanya biashara na Iran, mataifa ya dunia lazima yaelekee kwenye uhuru wa kiuchumi na kuondokana na Marekani."
Iran tayari imewasilisha malalamiko rasmi kwa Umoja wa Mataifa kufuatia matamshi ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ikimkosoa kwa kutoa vitisho vya kijeshi na kuwachochea waandamanaji kuteka taasisi za serikali.