Zoezi la kuhesabu kura Uganda linaendelea, Museveni anaongoza kwa zaidi ya 76%
-
Zoezi la kuhesabu kura Uganda linaendelea, Museveni anaongoza kwa zaidi ya 76%
Zoezi la kuhesabu kura nchini Uganda kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Alkhamisi ya jana linaendelea huku matokeo ya awali yakionyesha kuwa, Yoweri Museveni rais wa sasa anaongoza kwa wingi wa kura.
Matokeo ya awali ya uchaguzi nchini Uganda yanaonyesha Rais Yoweri Museveni akiongoza kwa zaidi ya asilimia 76 huku upinzani ukilalamikia udanganyifu, ghasia na mazingira ya ukandamizaji yaliyochagizwa na kuzimwa Intaneti.
Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais yanaonyesha Rais Yoweri Museveni akiongoza kwa mbali, huku kukiwa na simulizi zinazokinzana kuhusu ghasia zilizotokea baada ya upigaji kura. Uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira ya taharuki, usalama mkali na kukatwa kwa huduma ya intaneti nchini kote.
Tume ya Uchaguzi imetangaza kuwa, Museveni ana asilimia 76.25 ya kura baada ya takriban nusu ya kura za vituo vya kupigia kura kuhesabiwa. Mpinzani wake mkuu, mwanamuziki aliyekuwa maarufu kabla ya siasa Bobi Wine, alikuwa na asilimia 19.85 huku kura zilizobaki zikigawanywa kwa wagombea wengine sita.
Baada ya kupiga kura, Museveni aliwaambia waandishi wa habari kuwa alitarajia kushinda kwa karibu asilimia 80 iwapo kusingekuwa na udanganyifu. Kauli hiyo ilitafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kama ishara ya kujiamini kwa upande wa serikali.
Kwa upande mwingine, Bobi Wine alidai kuwepo kwa udanganyifu mkubwa katika mchakato mzima wa uchaguzi. Alitoa wito kwa wafuasi wake kupinga, akisema kizuizi cha mtandao kilitumika kuzuia ufuatiliaji wa makosa ya uchaguzi.
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema uchaguzi huo ulikuwa ukifanyika katika mazingira ya "ukandamizaji na vitisho vilivyoenea.” Umoja wa Mataifa pia ulionya kuwa ghasia za kisiasa katika nchi jirani ziliongeza hofu ya machafuko Uganda.