WFP: Mamilioni ya watu katika njaa kali Afrika Magharibi na Kati
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetoa onyo kali kutokea mjini Dakar, Senegal, likieleza kuwa bila rasilimali na hatua za haraka, watu walio katika mazingira magumu zaidi huko Afrika Magharibi na Kati wanakabiliwa na mwaka mwingine wa baa la njaa.
WFP inakadiriwa kuwa watu milioni 55 katika kanda hiyo watakumbwa na njaa kali ifikapo Juni hadi Agosti mwaka huu, huku zaidi ya watoto milioni 13 wakitabiriwa kuathirika na utapiamlo.
Katika taarifa iliyotolelwa Ijumaa, WFP imesema Hali hii inasababishwa na mchanganyiko wa mizozo inayozidi kuongezeka, watu kuhama makazi yao, na misukosuko ya kiuchumi. Hata hivyo, sababu kuu inayofanya hali kuwa mbaya zaidi ni kupungua kwa misaada ya kibinadamu kufuatia changamoto ya ufadhili.
Naibu Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika Magharibi na Kati, Sarah Longford, ameeleza uzito wa hali na kwa kubaini kuwa: “Misaada muhimu ya kibinadamu ni nguvu ya mabadiliko na utulivu katika mazingira tete. Kupungua kwa ufadhili tulikoshuhudia mwaka 2025 kumesababisha njaa na utapiamlo kuongezeka katika kanda nzima. Wakati mahitaji yanapozidi ufadhili, ndivyo hatari ya vijana kukata tamaa inavyoongezeka.”
Mataifa manne ya Afrika Magharibi Nigeria, Chad, Cameroon, na Niger yanachangia asilimia 77 ya takwimu hizi. Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu muongo mmoja, watu 15,000 katika jimbo la Borno nchini Nigeria wako katika hatari ya njaa ya kiwango cha juu zaidi cha IPC daraja la 5.
Sarah Longford ameongeza onyo kuhusu madhara ya njaa kwa usalama wa kanda akisema “Ni jambo la msingi tusaidie jamii zilizo katika mzozo, ili njaa iliyokithiri isichochee machafuko zaidi, ukimbizi, na mizozo katika kanda nzima.”
Sambamba na changamoto hizo, WFP imebainisha kuwa uwekezaji katika kujenga mnepo wa jamii una tija kubwa. Kwa mfano, urejeshaji wa ardhi katika eneo la Sahel huzalisha hadi dola 30 kwa kila dola moja inayowekezwa.
Hata hivyo, ili kuendelea kutoa misaada ya kuokoa maisha katika kipindi cha miezi sita ijayo, WFP inahitaji kwa dharura zaidi ya dola milioni 453 za Marekani.
Longford amehitimisha kwa kusema “Ili kuvunja mzunguko wa njaa kwa vizazi vijavyo, tunahitaji mabadiliko ya mfumo mwaka 2026. Serikali za kitaifa na washirika wao lazima waongeze uwekezaji katika kujiandaa, hatua za kutarajia majanga, na ujenzi wa uwezo wa jamii kujitegemea.”