UN yataka msaada wa haraka ufike Sudan kuepusha janga la kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135572-un_yataka_msaada_wa_haraka_ufike_sudan_kuepusha_janga_la_kibinadamu
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakimbizi na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, Barham Salih, ametoa wito wa dharura wa msaada wa kibinadamu na ulinzi kwa watu wanaokimbia vita vya kikatili nchini Sudan, akionya kuwa mgogoro huo sasa umekuwa janga kubwa zaidi na lenye athari mbaya zaidi la watu kufurushwa makwao duniani.
(last modified 2026-01-17T03:08:01+00:00 )
Jan 17, 2026 03:08 UTC
  • Barham Salih akiwa na wakimbizi wa Sudan
    Barham Salih akiwa na wakimbizi wa Sudan

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakimbizi na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, Barham Salih, ametoa wito wa dharura wa msaada wa kibinadamu na ulinzi kwa watu wanaokimbia vita vya kikatili nchini Sudan, akionya kuwa mgogoro huo sasa umekuwa janga kubwa zaidi na lenye athari mbaya zaidi la watu kufurushwa makwao duniani.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kwanza rasmi tangu ateuliwe  kuwa Kamishna Mkuu, Salih akiwa mjini N’Djamena amesema ukubwa wa mateso aliyoyaona miongoni mwa wakimbizi wa Sudan waliowasili hivi karibuni mashariki mwa Chad ni wa kusikitisha sana na unahitaji hatua za haraka kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Ameongeza kuwa: “Watu wanafika wakiwa hawana chochote isipokuwa majeraha ya kisaikolojia na hofu." Aidha amesema: “Wamepitia ukatili usioelezeka, kulazimika kufungasha virago mara kwa mara, na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Dunia haiwezi kupuuza mgogoro huu.”

Wakati wa ziara zake katika makazi ya wakimbizi nchini Chad, Salih amekutana na familia zilizokimbia mapigano makali huko Darfur siku chache tu zilizopita. Wengi wao walikuwa tayari wamefurushwa mara kadhaa tangu mgogoro huo uanze.

Wanawake wameelezea kubakwa, huku wengine wakisimulia kuuawa kwa wazazi na ndugu zao. Wengi waliwasili Chad wakiwa wamebeba tu kile walichoweza, wakitafuta usalama baada ya miaka ya hofu na vurugu.

Tangu vita vianze Sudan Aprili 2023, zaidi ya wakimbizi 900,000 wa Sudan wameingia mashariki mwa Chad, huku wageni wapya wakiendelea kuwasili kila siku.

Kwa ujumla, vita vya Sudan vimewasababisha watu milioni 12 kuhama makazi yao, wakiwemo zaidi ya wakimbizi milioni 4.3 katika eneo zima.

“Huu sasa ni mgogoro mkubwa zaidi wa watu kufurushwa makwao duniani,” amesisitiza Salih. “Nyuma ya takwimu hizi kuna watu halisi ambao maisha yao yamesambaratika.”

Ingawa UNHCR inaendelea kuongoza juhudi za kuokoa maisha nchini Chad, Salih ameonya kuwa upungufu wa fedha unazidi kudhoofisha operesheni za kibinadamu.

Familia nyingi za wakimbizi hazina makazi ya kutosha, upatikanaji wa maji uko chini sana ya viwango vya dharura, na vyoo vilivyojaa kupita kiasi vinaongeza hatari za kiafya. 

UNHCR imeongeza kuwa viwango vya msongo wa mawazo ni vya juu sana, lakini huduma za afya ya akili zinawafikia wachache tu kati ya wanaohitaji msaada. Maelfu ya watoto bado hawajaweza kurejea shuleni.

Mapigano ya Sudan yalianza Mwezi Aprili 2023 kati ya Jeshi la Kitaifa na waasi wa RSF wanaotaka kunyakua madaraka. Serikali ya Sudan inasema Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) unawasaidia waasi wa RSF. Hata hivyo, UAE imekanusha kuhusika.