Chad yaelemewa na wakimbizi wa Sudan, CAR, Cameroon, Nigeria na kwengineko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135582-chad_yaelemewa_na_wakimbizi_wa_sudan_car_cameroon_nigeria_na_kwengineko
Mzigo mkubwa wa wakimbizi wanaomiminika kila leo nchini Chad umeielemea serikali ya nchi hiyo ambayo muda wote inaiomba jamii ya kimataifa na hasa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR liisaidie kubeba mzigo huo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 17, 2026 04:40 UTC
  • Chad yaelemewa na wakimbizi wa Sudan, CAR, Cameroon, Nigeria na kwengineko

Mzigo mkubwa wa wakimbizi wanaomiminika kila leo nchini Chad umeielemea serikali ya nchi hiyo ambayo muda wote inaiomba jamii ya kimataifa na hasa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR liisaidie kubeba mzigo huo.

Taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa, Rais Mahamat Idriss Deby Itno ameonana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa Barham Ahmed Salih na kubadilishana naye mawazo kuhusu jinsi ya kuisaidia Chad kubeba mzigo huo. Mazungumzo hayo yalifanyika jana Ijumaa.

Katika taarifa yake rasmi, Ikulu ya Rais wa Chad imesema kuwa, Mahamat Deby ameelezea wasiwasi na kusikitishwa kwake na jinsi nchi yake ilivyobebeshwa mzigo huo peke yake kutokana na ufadhili mdogo wa jamii ya kimataifa na kuiweka Chad chini ya mzigo usiobebeka wa kuhudumia wakimbizi na wakati huo huo kukabiliana na magenge yenye silaha yanayojipenyeza nchini humo kwa jina la wakimbizi. Taarifa hiyo imesema kuwa, hivi sasa wakimbizi wanaunda takriban asilimia 44 ya idadi ya watu wa baadhi ya maeneo ya Chad hususan majimbo ya mashariki na hasa majimbo ya Ouaddai, Wadi-Fira, Sila na Ennedi Mashariki. Rais Mahamat Deby Itno amesema: "Jibu halipaswi tena kuwa msaada wa dharura, bali liwe ni msaada wa moja kwa moja wa kimuundo kwa ajili ya kuisaidia serikali yetu kubeba mzigo huu mkubwa."

Kwa upande wake, Barham Ahmed Salih amekiri kwamba mzigo wa wakimbizi inaobeba Chad ni mzito kwani wakimbizi hao wanamiminika nchini humo kutoka kila mpaka hasa kutokea Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nigeria, Cameroon na kwengineko. Taarifa hiyo imezungumzia pia suala la kuhamishiwa kambi za wakimbizi kwenye maeneo ya mpakani huku Rais Deby akiihimiza UNHCR itekeleze inavyopasa majukumu yake. Chad ndiyo nchi inayoongoza barani Afrika kwa kuhifadhi wakimbizi wengi zaidi. Rais wa Chad anasema, kuna karibu wakimbizi milioni 1.3 nchini humo hivi sasa.