Tume ya Uchaguzi Uganda: Yoweri Museveni ameshinda muhula wa saba wa urais
-
Yoweri Museveni
Tume ya uchaguzi nchini Uganda imemtangaza Yoweri Kaguta Museveni kama mshindi wa Uchaguzi wa Rais uliofanyika Alhamisi wiki hii, akiwa na jumla ya kura 7,946,772 ambayo ni asilimia 71.65% ya kura zote zilozopigwa.
Mpinzani wake wa karibu, Robert Ssentamu Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ameshika nafasi ya pili, akiwa na jumla ya kura 2,741,238 au asilimia 24.72%.
Kwa mujibu wa tume hiyo, kura 11,366,201 zilipigwa katika uchaguzi huu wa mwaka 2026, ikiashiria asilimia 52.50% ya idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki.
Ushindi wa Museveni uliotarajiwa na wengi unakuja baada ya kampeni ya uchaguzi ambayo Umoja wa Mataifa ulisema ilikumbwa na "ukandamizaji na vitisho", ikiwa ni pamoja na kukandamiza mikutano ya upinzani.
Bobi Wine, mwimbaji aliyegeuka kuwa mwanasiasa ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alidai kwenye mitandao ya kijamii siku ya uchaguzi kwamba "uchakachuaji mkubwa wa kura" ulikuwa ukifanyika.
Hata hivyo waangalizi wa uchaguzi wamesema leo Jumamosi kwamba hawakuona ushahidi wa kujazwa kura bandia kwenye masanduku ya kupigia kura lakini wameshutumu "ripoti za vitisho, kukamatwa na kutekwa nyara nyara" dhidi ya upinzani na mashirika ya kiraia.
Upinzani nchini Uganda pia umesema takriban watu 10 waliuawa na polisi katika shambulio dhidi ya nyumba ya mbunge wa eneo la Butambala, yapata kilomita 55 (maili 35) kusini magharibi mwa Kampala.
Ushindi wa Yoweri Museveni katika uchaguzi wa rais wa Uganda ulionekana kwa muda mrefu kama utaratiibu wa kimaonyesho tu, kwani mpiganaji huyo wa waasi wa zamani anadhibiti kikamilifu taasisi za serikali na vyombo vya usalama.
Tangu ashike madaraka ya nchi miongo minne iliyopita, Bwana Yoweri Museveni amebadilisha katiba mara mbili ili kuondoa ukomo wa umri na muda wa urais.
Chama chake tawala, National Resistance Movement, pia kilikuwa kikiongoza kwa kuwa na viti vingi vya Bunge, kwa mujibu wa matokeo ya muda. Kura za uchaguzi wa Bunge zilikuwa bado zinahesabiwa.