Rais wa Somalia atoa wito kwa Somaliland kushiriki katika mazungumzo
-
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia amewatolea wito maafisa wa Somaliland kushiriki katika mazungumzo na serikali yake; akisema kuwa yuko tayari kuafikiana katika masuala yote isipokuwa "umoja wa nchi."
Rais wa Somalia ameeleza haya alipotembelea Las Anod makao makuu ya uongozi ya jimbo ambalo jamhuri iliyojitenga ya Somaliland inadai pia kuwa milki yake. Hiyo ni ziara ya kwanza kufanywa katika eneo hilo na Rais wa Somalia katika kipindi cha zaidi ya miaka 40.
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia pia amesema hatua ya Israel ya kuitambua Somaliland imepingwa kimataifa na nchini Somalia akisisitiza kuwa umoja wa Somalia "hauwezi kujadiliwa."
Rais wa Somalia hivi karibuni alitembelea Las Anod makao makuu ya uongozi ya Sool kwa lengo la kuhudhuria katika hafla ya kuapishwa Rais wa jimbo jipya lililoasisiwa la kaskazini mashariki ambalo mwezi Agosti lilikuwa mwanachama wa sita wa shirikisho la Somalia.
Ofisi ya Rais wa Somalia imeitaja ziara hiyo kuwa ishara ya kuimarisha umoja na juhudi za serikali ya shirikisho kwa ajili ya mshikamano wa nchi hiyo na watu wake.
Disemba 26 mwaka jana, Israel ilitangaza kuitambua rasmi Somaliland kama taifa huru na lenye mamlaka kamili; hatua iliyopingwa na kukosolewa kikanda na kimataifa.