Afisa wa UN: Sudan 'imetumbukia katika shimo la mateso makubwa yasiyoelezeka'
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametahadharisha kuhusu kuzorota kwa hali ya haki za binadamu na kibinadamu nchini Sudan, kufuatia ziara yake ya siku tano katika nchi hiyo inayokumbwa na vita.
Akizungumza jijini Nairobi jioni ya Jumapili, Türk amesema Sudan “imetumbukia katika shimo la mateso makubwa yasiyoelezeka” kutokana na takribani miaka mitatu ya mapigano kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF). Ziara yake ilimfikisha Port Sudan, Dongola, pamoja na maeneo ya Ad Dabba na Merowe katika Jimbo la Kaskazini, ambako alikutana na wakimbizi wa ndani, viongozi wa jamii, wafanyakazi wa misaada, na maafisa wa serikali.
Türk amesema alishuhudia “ukatili usioelezeka” unaowakumba raia, huku akionya kuwa, ukatili kama ule uliofanyika wakati wa kuanguka kwa El Fasher unaweza kujirudia katika eneo la Kordofan, ambako mapigano yameongezeka.
Türk ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka hali ya kijeshi katika jamii ya Wasudan, ikiwa ni pamoja na kuajiri watoto na kuwapa raia silaha. Pia amekosoa kukamatwa kwa waandishi wa habari, wanasheria na wanaharakati wa kiraia kwa tuhuma za “kushirikiana” na pande pinzani, akisema vikwazo kwa vyombo vya habari vinachochea chuki na kuendeleza vita.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema “Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kufikiri kuwa kuendelea na mapigano ndiyo suluhisho," huku akibainisha masikitiko yake kuwa, “fedha nyingi zinatumika kununua silaha badala ya kupunguza mateso ya wananchi.”
Amewataka wahusika wa kikanda na wa kimataifa, hasa wale wanaotoa silaha au kunufaika kiuchumi na vita, kutumia ushawishi wao kusaidia kumaliza mgogoro huo.
Kama hatua ya haraka, Türk ametoa wito wa kulindwa kwa raia, kuruhusiwa kwa njia salama kwa watu wanaokimbia maeneo ya vita, kuruhusu misaada ya kibinadamu kufika bila vikwazo, kutendewa kwa kibinadamu kwa waliokamatwa, na kuachiliwa kwa raia wanaozuiliwa bila sababu za kisheria.
Mapigano nchini Sudan yalianza Aprili 2023 kati ya Jeshi la Serikali na waasi wa RSF wanaotaka kunyakua Madaraka. Serikali ya Sudan inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa ndie muungaji mkono mkuu wa waasi wa RSF wanaotenda jinai nchini humo.
Mapigano hayo yamesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya raia huku Wasudani karibu mamilioni 12 wakilazimika kuyahama makazi yao, na hivyo kuifanya Sudan kuwa moja ya maeneo yenye mgogoro mkubwa zaidi duniani..