Kwa nini nchi za eneo zinataka kudumishwa utulivu na uthabiti nchini Iran?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135630-kwa_nini_nchi_za_eneo_zinataka_kudumishwa_utulivu_na_uthabiti_nchini_iran
Machafuko ya hivi karibuni nchini Iran na tishio la Trump kuishambulia kijeshi Iran ikiwa ni katika madai ya kuwaunga mkono wanaojiita waandamanaji vimezifanya nchi za eneo kuwa na wasiwasi mkubwa.
(last modified 2026-01-18T10:52:12+00:00 )
Jan 18, 2026 10:52 UTC
  • Kwa nini nchi za eneo zinataka kudumishwa utulivu na uthabiti nchini Iran?

Machafuko ya hivi karibuni nchini Iran na tishio la Trump kuishambulia kijeshi Iran ikiwa ni katika madai ya kuwaunga mkono wanaojiita waandamanaji vimezifanya nchi za eneo kuwa na wasiwasi mkubwa.

Tovuti ya Daily Swabah imechapisha makala iliyoandikwa na Mustafa Janer mnamo Januari 15 chini ya kichwa kinachosomeka, "Ni Nani Wanataka Kuanguka Serikali Nchini Iran, ambapo amechunguza suala la machafuko ya hivi karibuni nchini na tishio la Trump kuishambulia kijeshi kwa madai ya kuwaunga mkono wanaojiita waandamanaji, na kusema jambo hilo limezua wasiwasi mkubwa katika nchi za eneo.

Miongoni mwa matukio makubwa yaliyotokea katika eneo katika miaka ya karibuni  ni wimbi la mwamko wa Kiislamu, ambalo lilibadilisha muundo wa kisiasa wa Asia Magharibi na Afrika Kaskazini na kutoa msingi wa kupanuka ushawishi wa Iran katika nchi kama vile Syria, Lebanon, Iraq na Yemen. Hali hii ilizifanya baadhi ya nchi za Kiarabu kuituhumu Iran kuwa ndiyo sababu ya kukosekana uthabiti, ambapo katika kipindi cha uongozi wa Donald Trump mashinikizo dhidi ya Tehran yalifikia kilele chake. Lakini baada ya janga la Corona na kupungua msaada wa Marekani kwa washirika wake wa kieneo, nchi kama Saudi Arabia, Imarati na Misri zilikabiliwa na changamoto mpya. Vita vya Ukraine pia vilichangia kukosekana amani duniani na kuongeza haja ya kuwepo utulivu katika eneo. Katika mazingira hayo, Iran na Saudi Arabia ziliamua kurekebisha uhusiano wao mnamo 2023, ambapo Uturuki pia iliboresha uhusiano wake na nchi za Kiarabu.

Matokeo ya Oktoba 7 na nafasi ya Israel 

Baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, 2023, Israel imedhihirika wazi kama chanzo muhimu zaidi cha ukosefu wa amani katika eneo hili. Mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon, Syria na Iran yametishia usalama wa eneo zima. Kukiuka ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni anga za nchi tofauti na hata kulengwa Qatar katika hali hiyo kunaonyesha kuongezeka mivutano katika eneo. Utawala wa Kizayuni umekuwa na nafasi kubwa katika matukio mengine ya ukosefu wa amani ikiwa ni pamoja na mgogoro wa Sudan, matukio ya machuafuko katika Pembe ya Afrika na kujitenga Somaliland. Utawala huu unapinga miundo thabiti ya kisiasa katika eneo na unanufaika na kudhoofika serikali katika nchi muhimu.

Kwa upande mwingine, nchi kama Uturuki, Saudi Arabia, Qatar na Misri zinataka kuimarisha serikali za kikanda na kuongeza uwezo wao wa kitaasisi. Nchi hizi zimewekeza nchini Syria na zimechukua misimamo inayofanana kuhusu matukio ya Sudan na Somaliland. Iran pia imeungana na Uturuki na Saudi Arabia katika masuala hayo.

Mazishi ya mashahidi waliouawa na magaidi katika ghasia za karibuni nchini Iran

Matukio ya Yemen na mashindano ya kikanda 

Operesheni za hivi karibuni za anga za Saudi Arabia zimetoa pigo kubwa kwa mipango ya Israel nchini humo. Mashambulio ya Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen yaliyojaribu kuvuruga mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Ansarullah ya Yemen yalichukuliwa kuwa tishio kwa usalama wa Riyadh. 

Majibu ya haraka ya Saudi Arabia yalionyesha kuwa nchi hii ina nia ya kukabiliana na mipango ya Israel katika Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu. Makubaliano ya karibuni ya ulinzi kati ya Uturuki, Saudi Arabia na Pakistan yanaweza pia kuchambuliwa katika mtazamo huo huo.

Maana ya kijiopolitiki ya machafuko ya Iran

Vyombo vya habari vya Magharibi vinamtambulisha Reza Pahlavi kama kiongozi wa waasi hao, lakini kiwango cha uungaji mkono halisi kwake ndani ya Iran kinatiliwa shaka. Uhusiano wake wa karibu na utawala wa Kizayuni, uungaji mkono wake kwa mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Iran na wafuasi wake kubeba bendera ya Israel, kunaashiria uhusiano wa ghasia hizo na utawala wa Tel Aviv. Baadhi ya vyombo vya habari hata vinachukulia kugawanywa Iran kama chaguo zuri zaidi kwa utawala wa Israel kuliko kurejea nchini kwa Pahlavi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameashiria mkono wa Israel nyuma ya pazia la machafuko nchini Iran, ambapo vyanzo vya Iran vimezungumzia ushirikiano wa kipelelezi na Uturuki dhidi ya makundi yanyotaka kujitenga kama vile Pejak. 

Waziri wa mambo ya nje wa Oman ametembelea Tehran nayo Saudi Arabia  inaendeleza mawasiliano ya kidiplomasia na Iran.

Kwa nini nchi za eneo hazitaki kuona Iran ikisambaratika?

Kimya cha nchi za Kiarabu, hususan serikali za Ghuba ya Uajemi, kinasababishwa na wasi wasi wa kuenea machafuko ndani ya mipaka yao, pamoja na hofu ya kuwa shabaha ya Iran, ikiwa itashambuliwa na Marekani. Lakini muhimu zaidi ni kwamba kusambaratika Iran kunaweza kusababisha migogoro mikubwa zaidi ambayo hakuna nchi yoyote inayoweza kuidhibiti kirahisi. Kwa maelezo hayo, karibu wahusika wote wa kieneo - isipokuwa utawala wa Kizayuni - wanataka kudumishwa utulivu na uthabiti nchini Iran.