UN yachunguza tuhuma za ubakaji za askari wake CAR
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa wameanza uchunguzi kuhusu tuhuma mpya zinazowakabili askari wa kulinda amani wa umoja huo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amesema umoja huo umeanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma mpya zinazowakabili askari wa kulinda amani wa umoja huo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati zikiwemo zile za ubakaji na kunajisi wanawake.
Uchunguzi huo ulianza siku kadhaa zilizopita na tayari maafisa wa Umoja wa Mataifa wamewasiliana na wenzao wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuhusu utambulisho wa watuhumiwa.
Farhan Haq amesema Umoja wa Mataifa tayari umewachukulia hatua askari wa kulinda amani wa umoja huo kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Congo Brazaville. Amesema kikosi cha askari wa kulinda amani cha Congo DR katika eneo na Bambari kitarejeshwa nyumbani tarehe 25 mwezi huu wa Februari na nafasi yao itachukuliwa na askari kutoka Mauritania.