Ukandamizaji wa sauti za kutetea Palestina nchini Ujerumani
Mauaji ya halaiki yanayoendelezwa na utawala wa Israel huko Gaza kwa kiasi kikubwa yamefutwa kwenye vyombo vya habari vya Ujerumani na katika ajenda ya umma; hata hivyo, ukandamizaji wa sauti za kuunga mkono Palestina haujatoweka.
Baada ya kupita zaidi ya miaka miwili na nusu tangu kuanza kwa mauaji hayo ya halaiki, Ujerumani bado inajaribu kunyamazisha sauti za wale wanaosimama kidete kupinga ukatili wa Utawala wa Kizayuni wa Israel na ubeberu huko Magharibi mwa Asia. Uvamizi wa nyumba, ukamatwaji, faini, na kupoteza ajira vimekuwa jambo la kawaida kwa wanaharakati watetezi wa Palestina.
Kaulimbiu zinapigwa marufuku, na watu wanashitakiwa ikiwa watapaza sauti katika maandamano wakisema: “Palestina ina haki ya kujitetea, hata kwa mawe na bunduki." Mamlaka za Ujerumani zinadai wenye kutetea Palestina wana uhusiano na harakati ya kupigania ukombozi wa Palestina, Hamas, ambayo imepigwa marufuku nchini humo. Wanaharakati wanakamatwa kwa kisingizo cha kuwa na uhusiano na Hamas.
Hali nchini Ujerumani ni ya maafa. Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limepokea ripoti kadhaa kuhusu vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza nchini humo. Uhuru wa kujieleza hauna maana yoyote tena kwa wale wenye madaraka Ujerumani.
Matthias Seipel, wakili, anasema: “Nchi iliyotenda mauaji ya halaiki dhidi ya Wayahudi, inaendelea kuunga mkono mauaji ya halaiki leo—huu ni mwendelezo wa kihistoria.”
Harakati za Mshikamano wa Palestina zinaonyesha jinsi serikali inavyotumia nyenzo zote katika ghala lake la ukandamizaji. Huko Frankfurt, kumekuwa na wimbi la tatu la uvamizi wa nyumba. Watu wanapoteza njia zao za kujipatia riziki.
Rabab Douwa anasema: “Tunashuhudia wenyewe nini maana yake wakati serikali inapounga mkono mauaji ya halaiki.”
Mohammad, mwanaharakati wa Palestina anayeishi Hanover, kaskazini mwa Ujerumani, amepoteza hadhi yake ya ukimbizi kutokana na harakati zake. “Ninakabiliwa na kufukuzwa kutoka Ujerumani. Sababu iliyotolewa ni kwamba harakati zangu zinanifanya kuwa hatari kwa jamii." Anaongeza kuwa: “Mimi nasimamia haki dhidi ya mauaji ya watoto yanayofanywa na Israel, na dhidi ya wimbi la ufashisti linaloongezeka.”
Mwaka jana, mamlaka mjini Berlin zilifuta uraia wa nchi mbili wa mwanamume mmoja Mpalestina mwenye uraia wa Ujerumani kutokana na harakati zake.
Tangu kuanza kwa vita vya Ukraine, mauaji ya halaiki yanayoendelea Gaza, pamoja na uchokozi wa kibeberu unaoendelea dhidi ya Lebanon na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mamlaka za Ujerumani zimezidisha hatua kali za ukandamizaji dhidi ya aina yoyote ya upinzani wa kisiasa.