Kenya yathibitisha kifo cha kwanza cha mgonjwa wa Ebola
-
Aden Duale, Waziri wa Afya wa Kenya
Kenya imethibitisha kisa chake cha kwanza cha Ebola na kifo cha kwanza kinachohusishwa na ugonjwa huo nchini, humo baada ya raia wa Kenya aliyekuwa akiishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufariki muda mfupi baada ya kurejea Nairobi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya Aden Duale, mgonjwa huyo alikuwa akiugua kwa takriban mwezi mmoja na alikuwa amepata matibabu nchini DRC kabla ya kusafiri kwa njia ya nchi kavu hadi Kampala, Uganda, na baadaye kusafiri kwa ndege kwenda Nairobi tarehe 3 Oktoba.
Duale amesema vipimo vilithibitisha kuwa alikuwa ameambukizwa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo na kwamba alifariki usiku wa Oktoba 5 akiwa chini ya uangalizi wa kitabibu.
Wizara ya Afya imetaja watu 28 waliokutana kwa karibu na marehemu, wakiwemo wanafamilia na wahudumu wa afya, na imesema uchunguzi na ufuatiliaji unaendelea. Serikali pia imewahakikishia wananchi kuwa hatua za kudhibiti maambukizi zimeimarishwa na hakuna visa vingine vilivyothibitishwa hadi sasa.
Kisa hicho kinatokea wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiendelea kukabiliana na mlipuko mkubwa wa Ebola uliotangazwa mwezi Mei. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuweko maelfu ya maambukizi na vifo vinavyohusishwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo, ambayo bado haina chanjo iliyoidhinishwa mahsusi wala tiba maalumu.
Kenya ilikuwa imeimarisha maandalizi ya kukabiliana na Ebola katika miezi ya karibuni kutokana na mlipuko unaoendelea katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Mamlaka za afya sasa zinaendelea na ufuatiliaji wa waliokutana na mgonjwa huyo ili kuzuia kuenea kwa maambukizi.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, dalili za Ebola zinaweza kuanza kuonekana kati ya siku mbili hadi 21 baada ya mtu kuambukizwa. Dalili za awali mara nyingi huanza ghafla na ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli na mwili, uchovu mkubwa, pamoja na maumivu ya koo.
Kadiri ugonjwa unavyoendelea, mgonjwa anaweza kupata kichefuchefu, kutapika, kuharisha, maumivu ya tumbo na upele kwenye ngozi. Katika hali kali, baadhi ya wagonjwa wanaweza kupata matatizo ya kutokwa damu ndani au nje ya mwili.