Kuakhirishwa duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa CAR
Duru ya mwisho ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ilipangwa kufanyika tarehe 31 mwezi huu imeakhirishwa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imetangaza kuwa duru ya mwisho ya uchaguzi wa Rais ambayo ilitazamiwa kufanyika siku ya Jumapili wiki ijayo imeakhirishwa kutokana na matatizo ya kimaandalizi.
Msemaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Julius Anguade Baba, ametangaza kuwa tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi ulioakhirishwa itatangazwa siku chache zijazo.
Wawakilishi wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na jamii ya kimataifa walichunguza kuhusu kuakhirisha duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo hadi tarehe 14 Februari katika kikao kilichofanya huko Bangui mji mkuu wa nchi hiyo. Pamoja na hayo yote, tarehe hiyo mpya bado haijathibitishwa.
Duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati imeakhirishwa huku wachambuzi wa mambo wakisema kuwa, raia wengi wa nchi hiyo na jamii ya kimataifa wanasubiri kufanyika uchaguzi na kutangazwa matokeo yake katika fremu ya kurejesha amani na utulivui nchini humo baada ya nchi hiyo kugubikwa na machafuko ya umwagaji damu mkubwa.
Mapigano nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo yalipamba moto kuanzia Disemba mwaka 2013, yalisababisha raia wengi wa nchi hiyo kuuawa na wengine zaidi ya milioni moja kuwa wakimbizi katika nchi jirani. Raia wengine wengi wa nchi hiyo wanaishi katika kambi za wakimbizi za Umoja wa Mataifa katika mazingira magumu. Japokuwa tangu awali, tarehe iliyoainishwa kwa ajili ya kufanyika uchaguzi huo ilikosolewa na kulalamikiwa na baadhi ya wasimamizi na weledi wa masuala ya kisiasa kutokana na maandalizi duni, lakini kwa kuzingatia hali iliyokuwa ikilegalega ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa upande mmoja, na kwa upande wa pili kuwepo ushawishi na uingiliaji wa baadhi ya nchi za Magharibi, uchaguzi wa Rais na Bunge wa nchi hiyo ulifanyika katika muda uliopangwa.
Kutofika masanduku ya kupigia kura katika baadhi ya ameneo ya uchaguzi na kuuzwa waziwazi karatasi za kura katika masoko huru ni miongoni mwa matatizo yaliyoripotiwa mwanzoni kabisa mwa zoezi la upigaji kura. Hata hivyo uchaguzi ulifanyika ulifanyika licha ya matatizo hayo yote. Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati tayari imebatilisha matokeo ya uchaguzi wa Bunge kutokana na matatizo hayo, hata hivyo mahakama hiyo imeidhinisha matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, uingiliaji wa nchi za Magharibi uliathiri maamuzi ya mahakama hiyo. Wachambuzi wengine wanaamini pia kuwa hatua ya Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ni sawa na kupuuza maamuzi ya wananchi katika uchaguzi huo na kwamba hatua hiyo tayari imeainisha matokeo ya uchaguzi. Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imeamua kwamba Anicet- Georges Dologuele na Faustin- Archange Touadera mdiyo wagombea wawili wa mwisho wa kiti cha urais watakaochuana katika duru ya pili. Suala hili pili limekosolewa na wachambuzi wa mambo kwa kutilia maanani kwamba wanasiasa wote hao wawili ni wanachama wa chama cha dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, François Bozizé.
Hali ya kisiasa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa mara yingine tena imebadilika kufuatia kuakhirishwa duru ya pili ya uchaguzi wa rais.
kwa sasa suala la kubadilishwa tarehe ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, kubatilishwa matokeo ya uchaguzi wa Bunge, kurefushwa muda wa vikwazo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hiyo vikiwemo vikwazo vya silaha kwa muda wa mwaka mmoja na kuendelea machafuko ya hapa na pale nchini humo, yote hayo kwa mara nyingine tena yametatiza matakwa ya wananchi waliotaka kufanyika haraka uchaguzi na kuundwa serikali ili kurejesha amani, umoja wa kitaifa na kuboresha hali ya uchumi wa nchi yao.