Kiongozi wa kanisa Kenya: Wanasiasa wanalifanyia siasa baa la njaa nchini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14236-kiongozi_wa_kanisa_kenya_wanasiasa_wanalifanyia_siasa_baa_la_njaa_nchini
Askofu wa Kanisa la Anglikana katika jimbo la Mombasa nchini Kenya Julius Kalu, amewakosoa vikali wanasiasa wa Pwani kwa kulifanyia siasa baa la njaa, ambalo limeathiri pakubwa baadhi ya maeneo ya eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2016 00:00 UTC
  • Kiongozi wa kanisa Kenya: Wanasiasa wanalifanyia siasa baa la njaa nchini

Askofu wa Kanisa la Anglikana katika jimbo la Mombasa nchini Kenya Julius Kalu, amewakosoa vikali wanasiasa wa Pwani kwa kulifanyia siasa baa la njaa, ambalo limeathiri pakubwa baadhi ya maeneo ya eneo hilo.

Askofu Kalu amewalaumu wanasiasa hao kwa kutojali maslahi ya wananchi ambao wameathiriwa na baa la njaa katika Kaunti za Kilifi na Kwale. “Tumeona wanasiasa wakijigamba kuwa wao wanajali maslahi ya watu na kufikia kuwazuia wapinzani wao kutotoa misaada ya vyakula katika maeneo yaliyoathiriwa. Watu wanakufa njaa huku viongozi wakijishughulisha na siasa.” Alisema kiongozi huyo wa kidini. Aidha amewalaumu wanasiasa hao kwa kuwafumba macho wananchi kwa kuwapa pesa ndogo ili kuwafanya waamini mambo wanayoyatekeleza ili waweze kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu ujao. 

Askofu Julius Kalu wa Mombasa, Kenya

Askofu Kalu ameongeza kwa kusema: “Kadri uchaguzi mkuu unavyokaribia ndivyo unavyoona wanasiasa wakitembelea sehemu hizo na kuwamiminia wakazi maji na vyakula. Bila kuwajibika wakati huu ambapo watu wameachwa wateseke kwa njaa kali. Ni jambo la aibu sana kuona wananchi wakiteseka kwa sababu ya njaa ilhali tuko na kila kinachohitajika kuwezesha watu wetu kupata chakula nchini.” Mwisho wa kunukuu. Amekosoa shughuli za maonyesho kwa kusema kuwa, ni suala la kusikitisha sana kuona maonyesho ya mwaka huu yanakuja wakati baa la njaa limeathiri maelfu ya wananchi katika baadhi ya sehemu ikiwemo Ganze, Bamba na Kinango nchini Kenya. Kufuatia hali hiyo ameiomba serikali ifanye juhudi kuhakikisha inawapatia mafunzo ya kilimo bora wakulima wa maeneo yaliyoathiriwa ili waweze kuyatumia katika kujipatia riziki na kuepuka njaa.