Polisi Mombasa yazima shambulio la kigaidi, wanawake watatu wauawa
Polisi ya Mombasa Kenya imetibua shambulio la kigaidi na kuwauwa wanawake watatu waliotaka kutekeleza shambulio hilo katika makao makuu ya polisi mjini humo.
Taarifa zinasema kuwa, wanawake watatu waliokuwa wamevaa mabaibui na walioaminika kuvaa mikanda ya kujilipua walivamia makao makuu ya polisi mjini Mombasa katika shambulio la kigaidi.
Maafisa wa polisi mjini Mombasa wanasema kuwa walitibua jaribio hilo na kufanikiwa kuwaua wanawake watatu huku wawili wakikamatwa.
Patterson Maelo Kamanda wa Polisi Kaunti ya Mombasa amesema kuwa, washukiwa hao waliwasili katika kituo cha polisi cha Central ili kuripoti tukio bandia la kuibiwa simu.
Wakati mashtaka yao yalipokuwa yakiandikishwa kituoni hapo mmoja wao alichukua kisu na kuwadungu maafisa wawili wa polisi huku mwingine akiwarushia polisi waliokuwa wakiandikisha malalamiko hayo bomu la petroli.
Polisi wanasema kuwa waliwafyatulia risasi na kuwaua wote.
Maafisa waliojeruhiwa wamepelekwa hospitalini huku kituo hicho cha polisi kikilindwa ili kuhakikisha kuwa hakuna tishio jingine linatokea.
Kumekuwa na mashambulio kadhaa katika eneo la pwani ya Kenya katika miaka ya hivi karibuni mengi yakifanywa na kundi la kigaidi la al-Shabab.