UN yaitaka Sudan Kusini ikubali kutumwa askari 4000 wa kieneo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17251-un_yaitaka_sudan_kusini_ikubali_kutumwa_askari_4000_wa_kieneo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka Sudan Kusini itekeleze ahadi iliyotoa, ya kukubali makubaliano ya kimataifa ya kutumwa askari 4,000 wa kieneo nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 12, 2016 04:10 UTC
  • UN yaitaka Sudan Kusini ikubali kutumwa askari 4000 wa kieneo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka Sudan Kusini itekeleze ahadi iliyotoa, ya kukubali makubaliano ya kimataifa ya kutumwa askari 4,000 wa kieneo nchini humo.

Ban Ki-moon amesema licha ya kwamba Juba ilikubali makubaliano hayo kwa matamshi, lakini hadi sasa imeshindwa kuonyesha kuridhika na makubaliano hayo kivitendo.

Wito wa Ban umejiri wiki moja baada ya Michael Makuei, Waziri wa Habari wa Sudan Kusini kutoa kauli ya kukinzana kuwa, Juba inahitaji ufafanuzi wa kutosha juu ya kutumwa askari hao wa kieneo.

Salva Kiir na Riek Machar

Licha ya serikali ya Sudan Kusini hivi karibuni kuafiki azimio la Umoja wa Mataifa wa kutumwa nchini humo wanajeshi elfu nne wa Kiafrika lakini imekuwa ikitoa kauli za kukinzana kuhusu suala hilo.

Mapigano nchini Sudan Kusini yalianza mwaka 2013 kati ya jeshi linalomuunga mkono Rais Salva Kiir na wanamgambo watiifu kwa aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar. Japokuwa mahasimu hao wakuu wa kisiasa walisaini hati ya makubaliano mwaka uliopita lakini amani na utulivu haujarejea tena nchini humo.

Maelfu ya watu waliuawa na mamia ya maelfu ya wengine kuuhama mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na kukimbilia maeneo mengine baada ya kuzuka mapigano kuanzia tarehe 8 hadi 11 za mwezi Julai mwaka huu baina ya askari watiifu kwa Rais Salva Kiir  na wapiganaji wanaomuunga mkono Riek Machar.