Salva Kiir awaonya wafanyao fujo Sudan Kusini
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amewaonya wafanyao fujo na wanaozusha machafuko ya kikabila nchini humo.
Salva Kiir alisema hayo jana mbele ya mamia ya wafuasi wa chama chake cha Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Sudan SPLM mjini Juba na kusisitiza kuwa, kama taasisi za kulinda usalama zitashindwa kurejesha utulivu nchini humo na iwapo zitashindwa kukomesha mauaji ya watu, basi atabeba yeye moja kwa moja jukumu la kupambana na machafuko hayo.
Amesema, kuna baadhi ya makundi ya watu wenye silaha yanaendesha vita na kusababisha ukosefu wa amani na usalama nchini humo, ili kuifanya Sudan Kusini idhibitiwe na vikosi vya kigeni.
Ameongeza kuwa, askari elfu nne wa Umoja wa Mataifa ambao mwezi Agosti mwaka huu walipasishwa na Baraza la Usalama la umoja huo kwa ajili ya kutumwa Sudan Kusini, hawawezi kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Wiki iliyopita serikali ya Sudan Kusini ilitangaza kuwa, tangu mwezi Septemba mwaka huu hadi hivi sasa, watu wasiopungua 95 wamekuwa wahanga wa machafuko katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Aidha ilisema, lengo la makundi yanayoendesha machafuko hayo ni kushadidisha mizozo ya kikabila na kuandaa mazingira ya kudhibitiwa Sudan Kusini na majeshi ya kigeni.