Kenya yapiga marufuku kutoka nje usiku mjini Mandera
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18292-kenya_yapiga_marufuku_kutoka_nje_usiku_mjini_mandera
Serikali ya Kenya imetangaza marufuku ya kutotembea majira ya usiku kwa muda wa siku 60 eneo la Mandera, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 28, 2016 01:09 UTC
  • Kenya yapiga marufuku kutoka nje usiku mjini Mandera

Serikali ya Kenya imetangaza marufuku ya kutotembea majira ya usiku kwa muda wa siku 60 eneo la Mandera, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya, Joseph Ole Nkaissery imesema kuwa, amri hiyo imekuja kufuatia mji huo kushudia mashambulizi ya mauaji yaliyofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la ash-Shabab. Ameongeza kuwa, amri ya kutotembea majira ya usiku, itaendelea hadi tarehe 27 Disemba mwaka huu katika mji wa Mandera. Itakumbukwa kuwa Jumanne iliyopita, wanachama wa kundi hilo la kigaidi, walifanya shambulizi dhidi ya hoteli moja ya mji huo na kuua watu 12 na kujeruhi wengine kadhaa. 

Wanachama wa ash-Shabab nchini Somalia wanaohusika na hujuma za kigaidi nchini Kenya

Mkuu wa Polisi ya eneo la Mandera Mashariki, Ezekiel Singoe alinukuliwa akisema kuwa, wanamgambo hao wa ash Shabaab walivamia Hoteli ya Bishaaro mjini Mandera na kuwaua kwa kuwafyatulia risasi watu 12 wakiwemo 10 ambao si wakazi wa eneo hilo. Shambulizi hilo ni la pili kufanywa ndani ya kipindi cha chini ya wiki tatu baada ya hujuma nyingine kama hiyo kufanywa na wanachama wa genge hilo kwenye eneo hilo. Wanachama wa ash-Shabab wametangaza vita dhidi ya serikali ya Nairobi kuwa kushiriki katika operesheni za kijeshi za askari wa kusimamia Amani wa Umoja wa Afrika AMISOM, nchini Somalia.