Feb 24, 2016 07:36 UTC
  • Ban Ki-moon atembelea kambi ya wakimbizi Goma, DRC

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon baada ya kutoka Burundi ameelekea Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo ametembelea kambi ya wakimbizi.

Akiandamana na mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo Maman Sidiku na Gavana wa Kivu Kaskazini Julien Paluku, Ban ametembelea kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kitchanga.

Kambi hiyo ni makazi ya wakimbizi wapatao 15,000 waliokimbia mapigano Kivu Kaskazini. Kambini humo Bwana Ban ametemebelea duka la kuuza mikate, shule ya msingi na kukutana na kikundi cha wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari kambini Kitchanga, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa usaidizi wa kibinadamu kwa watu wanaoteseka zaidi kwa kusema:

“Yote niliyoyasikia nimeyaona mwenyewe. Nimeguswa sana. Kama Katibu Mkuu, nataka kukutana na walioteseka zaidi. Nataka kuwa mtetezi wao; sauti ya wale waliokosa sauti. Nadhani tunapaswa kuimarisha usaidizi wa kibinadamu. Ndio maana ninaitisha kongamano la kwanza la kimataifa kuhusu masuala ya kibinadamu mjini Istanbul, mwezi Mei.”

Baada ya kuzuru kambi ya Kitchanga, Ban alikutana ana kwa ana na Daktari Denis Mukwege aliyeshinda tuzo ya kimataifa kwa juhudi zake katika kupambana na ukatili wa kingono DRC. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye alianza safari yake barani Afrika kwa kuitembelea Burundi sasa yuko Kinshasa ambapo amekutana na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tags