Nov 01, 2016 07:47 UTC
  • Kuchunguzwa tuhuma za ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia Nigeria

Rais wa Nigeria ameamuru kuchunguzwa tuhuma zilizowasilishwa dhidi ya wanajeshi wa nchi hiyo kwamba waliwabaka na kuwadhalilisha kijinsia wanawake na mabinti katika kambi za wakimbizi nchini humo.

Rais Muhammad Buhari jana aliagiza kuchunguzwa tuhuma zilizowasilishwa na Human Rights Watch kuwa wanajeshi na polisi wa nchi hiyo waliwabaka na kuwadhalilisha kijinsia wanawake na mabinti katika kambi za wakimbizi nchini humo. Rais wa Nigeria ameeleza kushangazwa na na kutiwa wasiwasi na vitendo hivyo  na akasema amewaagiza viongozi wa ngazi ya juu wa polisi na wakuu wa mikoa kuchunguza haraka tuhuma hizo.

Raia wa Nigeria waliokimbia hujuma za Boko Haram wakiwa kambini huko Dikwa

Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema kuwa askari usalama wa Nigeria wamewabaka na kuwadhalilisha kijinsia wanawake na mabinti wanaokimbia mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika eneo lililoathiriwa na machafuko la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Shirika hilo jana lilibainisha katika taarifa yake kuwa, kesi za udhalilishaji wa kijinsia zisizopungua 43 ukiwemo ubakaji na kuwatumia kingono zilisajiliwa na watafiti wa shirika hilo mwezi Julai mwaka huu.

 

 

Tags