Somalia na UN zakaribisha usitishaji mapigano baina ya Puntland na GalMudug
-
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia
Rais wa Somalia na mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo wamekaribisha makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyofikiwa baina ya majimbo mawili ya nchi hiyo ya Puntland na GalMudug juu ya eneo la Galkayo.
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia na mjumbe wa UN katika masuala ya nchi hiyo Michael Keating, jana walitoa taarifa mjini Mogadishu ya kupongeza makubaliano yaliyosainiwa baina ya Rais wa Jimbo la Puntland Abdiweli Mohamed Ali Gaas na mwenzake wa GalMudug Abdikarim Hussein Guled ya kumaliza mgogoro na machafuko katika eneo la Galkayo.
Keating amesema kusainiwa makubaliano hayo ni hatua chanya na kuzitaka pande mbili kuyaheshimu kwa kukomesha machafuko na kusaidia wakimbizi warejee makwao.
Kwa upande wake, Rais Hassan Sheikh Mohamud ametoa wito kwa viongozi wa majimbo hayo kutekeleza haraka makubaliano kuhusiana na eneo la Galkayo na kusisistiza kuwa serikali ya shirikisho iko tayari kusaidia pande zote mbili za Puntland na GalMudug ili kufanikisha utekelezaji wa makubaliano hayo ambayo yamesainiwa Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita watu zaidi ya 20 wakiwemo raia waliuawa na wengine zaidi ya 80 elfu walilazimika kuhama makazi yao kufuatia mapigano baina ya vikosi vya majimbo mawili ya Puntland na GalMudug.../