OCHA: Watu karibu milioni tatu Sudan Kusini wamekuwa wakimbizi tangu 2013
Ofisi ya uratibu ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya kibinaadamu (OCHA) imeetangaza kuwa, karibu watu milioni tatu raia wa Sudan Kusini wamekuwa wakimbizi wa ndani au katika nchi jirani tangu mwezi Disemba mwaka 2013 hadi sasa.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya OCHA imesema kuwa kwa mujibu wa takwimu ilizonazo, jumla ya watu milioni moja na laki nane na 70 elfu raia wa nchi hiyo wamekuwa wakimbizi wa ndani. Imeongeza kuwa, wengi wa wakimbizi wa machafuko na ukatili ndani ya taifa ghilo wamekimbilia eneo la Greater Equatoria, baada ya kuyahama makazi yao. Aidha ofisi ya uratibu ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya kibinaadamu imesema idadi ya wakimbizi wa Sudan Kusini wa eneo la Central Equatoria, imeongezeka mara mbili zaidi.
Kabla ya hapo John Ging, mkuu wa kitengo cha operesheni za masuala ya binaadamu ya Umoja wa Mataifa, alitahadharisha juu ya hali mbaya ya kibinaadamu nchini Sudan Kusini kutokana na mgohoro wa chakula na changamoto za kiuchumi nchini humo. Machafuko na mgogoro wa kisiasa nchini humo, uliibuka mwezi Disemba mwaka 2013, ikiwa ni miaka miwili tu tangu taifa hilo changa zaidi barani Afrika lijitenge na Sudan.