Timu ya upatanishi yaelekea Gambia kusuluhisha mzozo wa urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21334-timu_ya_upatanishi_yaelekea_gambia_kusuluhisha_mzozo_wa_urais
Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf anaongoza timu ya upatanishi inayotazamiwa kuelekea nchini Gambia hii leo kujaribu kuupatia ufumbuzi mzozo wa uongozi ulioibuka nchini humo, baada ya Rais Yahya Jammeh kupinga matokoe ya uchaguzi wa rais.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 13, 2016 08:13 UTC
  • Timu ya upatanishi yaelekea Gambia kusuluhisha mzozo wa urais

Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf anaongoza timu ya upatanishi inayotazamiwa kuelekea nchini Gambia hii leo kujaribu kuupatia ufumbuzi mzozo wa uongozi ulioibuka nchini humo, baada ya Rais Yahya Jammeh kupinga matokoe ya uchaguzi wa rais.

Adama Barrow aliyetangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, timu hiyo ya upatanishi inajumuisha marais na viongozi kadhaa wa kieneo.

Amesema lengo la jopo hilo kwenda nchini Gambia ni kuhakikisha kuwa Jammeh anaheshimu matakwa ya wananchi kwa kuyakubali matokeo ya uchaguzi bila ya masharti yoyote na kukabidhi madaraka kwa rais aliyechaguliwa.

Yahya Jammeh, aliyepinga matokeo ya uchaguzi wa rais Gambia

Hii ni katika hali ambayo, siku chache zilizopita Jammeh alizuia ndege iliyombeba Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Banjul, ambapo mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Uchumi ya Magharbi mwa Afrika (ECOWAS), alitumwa nchini humo kufuatilia mgogoro huo wa uchaguzi.

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zimemtaka Jammeh akubali matokeo ya uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo mwanzoni mwa mwezi huu, ambapo mpinzani wake Adama Barrow alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 43.29 ya kura kulinganisha na asilimia 39.64 aliyopata Yahya Jammeh. Awali kiongozi huyo aliyetawala Gambia kwa zaidi ya miaka 20 aliyakubali matokeo hayo na kukiri kushindwa.  

Adama Barrow, Rais mteule wa Gambia akihutubia wafuasi wake

Kuhusu iwapo anaunga mkono wazo la suluhisho la kijeshi, Adama Barrow amesema yeye binafsi na wananchi walio wengi wanataka kuona kuwa misingi ya demokrasia na amani inadumishwa nchini humo na kuongeza kuwa, binafsi kama rais mteule, maisha yake yamo hatarini kwa kuwa hajapewa mlinzi hadi sasa.