Umoja wa Mataifa watoa wito wa maridhiano ya kitaifa Libya
Umoja wa Mataifa sanjari na kuvipongeza vikosi vitiifu vya Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya kwa kuudhibiti kikamilifu mji wa pwani wa Sirte na kuukomboa kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Daesh, umewataka wananchi wote wa nchi hiyo kushirikiana katika mchakato wa maridhiano ya kitaifa.
Akiongea jana (Jumapili) mbele ya waandishi wa habari huko Tunis, mji mkuu wa Tunisia, Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya, Martin Kobler amesema taifa la Libya linafaa kutumia fursa na ushindi huo mkubwa dhidi ya magenge ya kigaidi mjini Sirte, kufikia maridhiano ya kitaifa.
Amesema kukombolewa mji wa Sirte ni hatua moja mbele ya kuikomboa Libya nzaima kutoka kwenye makucha ya makundi ya kigaidi, huku akiwataka Walibya kuwa macho kutokana na harakati za magenge hayo hatari.
Martin Kobler amesema kuna haja ya kutangamana na kuwapeleka katika vituo maalumu vya ushauri nasaha wapiganaji pamoja na kuanza shughuli ya kukusanya silaha zilizokuwa mikononi mwa magaidi.
Siku ya Jumamosi, Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilitangaza kumalizika operesheni ya kukomboa mji wa Sirte iliyodumu kwa takribani miezi saba baada ya ushindi wa jeshi la Libya, hatua inayohesabiwa kuwa ni pigo kubwa kwa kundi la Daesh katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Mji wa Sirte uliokuwa ukihesabiwa kuwa ngome ya mwisho muhimu ya kundi la kigaidi la Daesh nchini Libya kwa takriban mwaka mmoja sasa, umekombolewa kwa gharama ya kuuawa wanajeshi takribani 700 wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya nchi hiyo.