Feb 29, 2016 15:23 UTC
  • Buhari: Kuendelea kushuka bei ya mafuta duniani, hakukubaliki

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, amesema kuwa kuendelea kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, ni jambo lisilokubalika.

Rais Buhari ameyasema hayo leo Jumatatu na kuongeza kuwa, wanachama wote wa Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) na wale wasiokuwa wanachama wa jumuiya hiyo, kwa pamoja wanatakiwa kushirikiana ili kurejesha uthabiti wa bei ya mafuta ghafi duniani. Sanjari na kuashiria kuwa, ushirikiano wa pamoja wa wanachama utasaidia kupatikana uthabiti katika soko la mafuta ghafi duniani, Buhari amesema kuwa suala hilo litawasaidia wananchi wa maeneo yote ya dunia na kuwa, hali ya sasa katika soko la dunia haikubaliki kabisa. Kwa miaka miwili sasa Saudia imevuruga bei ya mafuta duniani kutoka Dola 110 kwa pipa na kufikia kiasi cha chini ya Dola 50, kwa lengo la kutoa pigo kwa uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Iraq, suala ambalo limekuwa na taathira mbaya kwa uchumi wa nchi nyingi, ikiwemo Saudia yenyewe ambayo sasa inakabiliwa na tishio la kufilisika. Kwa sasa bei ya kila pipa katika Jumuiya ya (OPEC) ni Dola 29.48. Nchi za Algeria, Angola, Ecuador, Libya, Kuwait, Nigeria, Qatar, Iran, Saudia na Venezuela, ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC).

Tags