Onyo la Ban kuhusu uwezekano wa kutokea mauaji ya kimbari Sudan Kusini
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeondoka Ban Ki-Moon ameonya kuhusu uwezekano wa kuibuka mauaji ya kimbari Sudan Kusini iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Akihutubu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu, Ban amelitaka baraza hilo kuweka vikwazo vya silaha dhidi ya nchi hiyo.
Wiki iliyopita pia Mjumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini alisema maeneo kadhaa ya nchi hiyo yameshuhudia matukio ya uangamizaji wa kikabila.
Yasmin Sooka, aliyasema hayo baada ya safari yake nchini Sudan Kusini na kubainisha kuwa, mazingira yaliyopo nchini humo hivi sasa yanafanana na yale yaliyokuwepo nchini Rwanda kabla ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Alifafanua kuwa, uangamizaji wa kikabila umekuwa mwenendo unaoendelea nchini Sudan Kusini na kwamba kuna uwezekano hali hiyo kugeuka na kuwa mauaji ya kimbari.
Sudan Kusini ilipata uhuru baada ya kujitenga na Sudan mwaka 2011 na kutumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. Makumi ya maelfu ya watu wameuawa hadi sasa katika mapignao ya makabila hayo mawili huku watu wengine milioni tatu wakilazimika kuwa wakimbizi.
Machar hivi sasa yuko uhamishoni Afrika Kusini na kunafanyika jitihada za kimataifa kurejesha amani katika nchi hiyo changa zaidi duniani.