Umasikini wapungua Kenya kupitia huduma za pesa kwa simu za mkononi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22936-umasikini_wapungua_kenya_kupitia_huduma_za_pesa_kwa_simu_za_mkononi
Kenya imefanikiwa kupunguza umasikini nchini humo kwa kueneza utumizi wa huduma za pesa kwa simu za mkononi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 06, 2017 04:39 UTC
  • Umasikini wapungua Kenya kupitia huduma za pesa kwa simu za mkononi

Kenya imefanikiwa kupunguza umasikini nchini humo kwa kueneza utumizi wa huduma za pesa kwa simu za mkononi.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa hivi karibuni na Jarida la Science, kuna athari za muda mrefu za kiuchumi zinazotokana na kuwawezesha wananchi kutumia mfumo huo wa kifedha.

Uchunguzi umebaini kuwa ongezeko la utumizi wa huduma za pesa kwa simu za mkononi umechangia kupunguza umasikini Kenya hasa miongoni mwa nyumba zinazosimamiwa na kuendeshwa na wanawake. Uchunugzi huo umesema kuenea kwa kasi huduma za pesa kwa simu za mkononi kumepelekea asilimia mbili ya familia za Kenya (yaani familia 194,000) kujikwamua kutoka katika umasikini wa kupindukia. Aidha huduma hizo zimewawezesha wanawake 185,000 kujistawisha kutoka kilimo cha kujikimu  hadi biashara zenye kuleta faida na pato bora.

Abiria akilipa nauli katika matatu kwa kutumia simu ya mkononi

Benki ya dunia inasema Kenya inaongoza duniani kwa mfumo wa kutuma na kupokea pesa kwa simu za mkononi. Mfumo huo ambao sasa ni maarufu kama M-PESA ulianzishwa na shirika la simu la Safaricom mwaka 2007 na hivi sasa kuna watu zaidi ya milioni 19  wanaotumia mfumo huo nchini humo na kubadilishana Shilingi bilioni 15 kwa siku kupitia mfumo huo. Huduma hizo zinatumiwa kulipa mishahara, huduma kama vile umeme, nauli, unuzi wa bidhaa n.k. Hivi karibuni  kampuni ya kimataifa ya Apple ilisema inapanga kupeleka nchini Kenya malipo kwa mfumo wa dijitali, Apple Pay. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Apple Pay kuingia barani Afrika ambapo itamenyana na mifumo mengineyo ya malipo iliyokita mizizi nchini humo hasa M-PESA.