Madaktari nchini Kenya wakataa nyongeza ya mishahara ya Rais Kenyatta
Madaktari nchini Kenya wamekataa nyongeza ya karibuni zaidi iliyopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta ikiwa ni katika juhudi za kujaribu kumaliza mgomo wa madaktari na wahudumu wa afya ambao umedumu kwa mwezi mmoja sasa.
Madaktari na wauguzi wa Kenya wametangaza kuwa, hawakubaliani na nyongeza hiyo na kwamba, wataendelea na mgomo wao hadi pale matakwa yao yatakapotekelezwa kikamilifu.
Rais Uhuru Kenyatta alikutana na wawakilishi wa chama cha taifa cha madaktari hao Jumanne na kupendekeza nyongeza ya mshahara na marupurupu ya madaktarii kwa angalau takribani shilingi milioni mbili kutoka kiwango cha sasa cha karibu shilingi milioni moja na nusu.
Hata hivyo, madaktari kwa upande wao wanaitaka serikali ya Rais Uhuru Kenyatta itekeleze makubaliano ya mishahara na marupurupu yaliyotiwa saini kati ya pande mbili mwaka 2013.
Kwenye makubaliano hayo, pamoja na mambo mengine serikali ya Kenya iliahidi kuongeza idadi ya madaktari, kuongeza pesa za utafiti wa kimatibabu, marupurupu kwa wafanyakazi wa sekta hiyo, dawa na vifaa na mitambo katika hospitali za umma.
Mgomo huo umeathiri huduma kwenye hospitali za umma huku wafanyakazi wa sekta ya umma wakidai kuwa lazima serikali iheshimu utekelezaji wa mkataba uliotiwa sahihi mwaka 2013. Makumi ya wagonjwa wameshafiriki dunia tangu mgomo huo ulipoanza mwezi mmoja uliopita.
Viongozi wa upinzani nchini Kenya wanamkosoa vikali Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa kushindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro huo na kutekeleza matakwa ya wafanyakazi hao katika moja ya sekta muhimu kabisa nchini humo.