UN: 50,000 wameuawa katika mapigano ya Sudan Kusini tangu 2013
Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya 50,000 wameuawa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Afisa mwandamizi wa umoja huo ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, hali ya Sudan Kusini inatisha na kwamba mbali na mauaji hayo ya watu zaidi ya 50,000, watu wengine zaidi ya milioni 2.2 wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi kutokana na mgogoro huo ulioanza Disemba mwaka 2013. Ofisa huyo wa Umoja wa mataifa ameongeza kuwa, zaidi ya watu laki 2 wa Sudan Kusini kwa sasa wanapatiwa hifadhi katika kambi 6 za vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini humo.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini mwaka 2013 alimuuzulu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar, suala ambalo lilianzisha hitilafu kubwa za kisiasa kati ya pande hizo mbili. Baada ya hapo kulitokea vita kati ya jeshi la Sudan Kusini na waasi wakiongozwa na Riek Machar ambavyo vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu. Mwezi Agosti mwaka jana pande hizo mbili zilifikia makubaliano ya amani chini ya mashinikizo ya kieneo na kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, Sudan Kusini imekubaliwa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.