Barrow ataka sherehe za kuapishwa kwake zifanyike kama ilivyopangwa, Gambia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23779-barrow_ataka_sherehe_za_kuapishwa_kwake_zifanyike_kama_ilivyopangwa_gambia
Rais mteule wa Gambia amesema kuwa, sherehe za kuapishwa kwake kama rais mpya wa nchi hiyo zinapaswa kufanyika kama ilivyopangwa.
(last modified 2025-10-22T13:08:56+00:00 )
Jan 18, 2017 04:10 UTC
  • Barrow ataka sherehe za kuapishwa kwake zifanyike kama ilivyopangwa, Gambia

Rais mteule wa Gambia amesema kuwa, sherehe za kuapishwa kwake kama rais mpya wa nchi hiyo zinapaswa kufanyika kama ilivyopangwa.

Adama Barrow ambaye kwa sasa yuko nchini Senegal, amesema sherehe za kuapishwa kama rais mpya wa Gambia zinapaswa kufanyika Alkhamisi ya tarehe 19 Januari kwa mujibu wa katiba ya Gambia. 

Barrow amelaani kitendo cha serikali ya Rais Yahya Jammeh cha kuwatia nguvuni askari polisi na raia wa kawaida na ametoa wito wa kuachiwa huru watu hao.

Wakati huo huo Morocco imetangaza kuwa imeanza mchakato wa kupatanisha katika mgogoro wa uchaguzi nchini Gambia.

Mgogoro huo ulianza baada ya Rais wa sasa wa nchi hiyo, Yahya Jammeh kukataa matokeo ya uchaguzi wa rais ambayo yalimpa ushindi mpinzani wake, Adama Barrow.

Rais Jammeh anaendelea kung'ang'ania madaraka Gambia

Nigeria na nchi kadhaa za Afrika Magharibi zimetishia kutuma nguvu za jeshi kumuondoa madarakani Rais Yahya Jammeh iwapo hatakabidhi madaraka ifikapo tarehe 19 mwezi huu.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika pia limetangaza kwamba tangu tarehe 19 mwezi huu wa Januari halitamtambua tena Yahya Jammeh kama Rais wa Gambia.