Mar 04, 2016 14:40 UTC
  • Wanaigeria waandamana wakitaka kuachiwa huru Sheikh Zakzaky

Wananchi wa Nigeria wameandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kuachiwa huru haraka kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo (IMN) Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Maandamano hayo yalifanyika jana katika mitaa ya miji kadhaa ikiwemo ya Kano, Kaduna na Yola ambapo wananchi walimiminika kwa wingi wakilalamikia hatua ya hivi karibuni ya jeshi la Nigeria ya kuwaua Waislamu wa Kishia na vile vile kuendelea kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky na wanachama wengine wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Wafanya maaandamano hayo wameitaja hatua ya kufungwa jela Sheikh Zakzaky na wafuasi wake kadhaa kuwa kinyume na katiba ya Nigeria. Abduhamid Bello Msemaji wa Tawi la Vijana la Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambalo ndilo lililoandaa maandamano hayo amesema kuwa wafuasi wa harakati hiyo wataendelea kufanya maandamano ya amani ili kufuatilia matakwa yao. Itakumbukwa kuwa tarehe 12 Disemba mwaka jana vikosi vya Nigeria vilishambulia marasimu ya kidini ya Waislamu wa Kishia katika mji wa Zaria na kuwatuhumu kuwa walizuia msafara wa mkuu wa jeshi na pia kujaribu kumuua, madai ambayo yamekanushwa na Waislamu hao.

Tags