Mgogoro wa Libya; ajenda kuu ya mazungumzo ya kieneo na kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24795-mgogoro_wa_libya_ajenda_kuu_ya_mazungumzo_ya_kieneo_na_kimataifa
Huku mgogoro wa kisiasa ukiendelea huko Libya, mashauriano ya kulipatia ufumbuzi tatizo la nchi hiyo yameendelea huko Malta kwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi kutoka nchi jirani na vile vile Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2017 00:32 UTC
  • Mgogoro wa Libya;  ajenda kuu ya mazungumzo ya kieneo na kimataifa

Huku mgogoro wa kisiasa ukiendelea huko Libya, mashauriano ya kulipatia ufumbuzi tatizo la nchi hiyo yameendelea huko Malta kwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi kutoka nchi jirani na vile vile Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Libya.

Hii ni katika hali ambayo Jenerali Khalifa Haftar Kamanda wa Jeshi la Libya mashariki mwa nchi ametahadharisha kuhusu uingiliaji wa jamii ya kimataifa katika masuala ya ndani ya Libya na kusisitiza kuwa wananchi wa nchi hiyo wenyewe wanaweza kujiamulia mustakbali wa nchi yao. Waziri Mkuu wa Ubelgiji alisema katika kikao kilichofanyika hivi karibuni huko Malta kuwa serikali ya Libya haina uwezo wa kulinda usalama wa mipaka yake na kwamba kukiongezea uwezo wa kisuhula na kifedha na kukipatia mafunzo kikosi cha ulinzi cha pwani ya nchi hiyo ili kilinde umoja wa kitaifa na hatimaye kuwazuia wahajiri wanaoelekea Ulaya, ni miongoni mwa vipaumbele vya Umoja wa Ulaya.

Charles Michel, Waziri Mkuu wa Ubelgiji 

Nchi za Ulaya hivi sasa zimeazimia kutatua tatizo la wahajiri kupitia nchi ambazo wahajiri wanatoka na kwa kustafidi na mpango unaoshabihiana na ule wa Utururiki.  Hii ni katika hali ambayo, hali ya mambo katika nchi kama Libya kimsingi si ya utulivu. Magenge ya magendo ya binadamu yanaendesha shughuli zake wazi wazi katika mipaka na pwani ya nchi hiyo. Suala hilo sambamba na kuwepo hatari ya kurejea tena magaidi na vile vile kuporwa maliasili na akiba kubwa ya mafuta ya nchi hiyo limedhoofisha sana  hali ya mambo ya Libya kuliko wakati mwingine wowote na hivyo kutoa mwanya kwa nchi ajinabi kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo kwa visingizio mbalimbali. Libya ambayo inakabiliwa na hali ya mchafukoge na ugaidi inakabiliwa pakubwa na mashinikizo ya ndani. Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ilitumbukia katika dimbwi la matatizo mara baada ya kuanza mgogoro wa kisiasa nchini humo kufuatia kupinduliwa madarakani Muammar Gaddafi dikteta wa zamani wa nchi hiyo mwaka 2011. Hali ya nchi hiyo imezidi kuwa tata kutokana na ukosefu wa amani na hujuma za makundi ya kigaidi zinazoendelea kuitatiza nchi hiyo kila uchao. Changamoto hizo zote zimezidisha shaka kuhusu kufanikiwa mpango wa kuwazuia wahajiri huko Libya.  Katika upande mwingine huko Ulaya pia hali inatia wasiwasi. Tuhuma za ugaidi zinazonasibishwa kwa wahajiri zimezidisha harakati za vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo mikali katika nchi nyingi za Ulaya. Jambo hilo limezidisha uwezekano wa kuingia madarakani vyama vya mrengo huo vyenye misimamo ya kufurutu ada chini ya shaari za uzalendo na kupinga wahajiri barani Ulaya. Katika mazingira hayo, nchi za Ulaya zina chaguo moja tu la kimantiki la kuziwezesha kuepuka hali hiyo ya mgogoro. Zinapasa kuwajibika kwa kutatua mizozo na vita vilivyopelekea kudhihiri wimbi hilo la wahajiri. Vita vinavyoendelea huko Syria na Iraq, mapigano  huko Libya na mizozo mingine ya silaha ni miongoni mwa sababu kuu za kuibuka na kushtadi mgogoro wa wakimbizi; ambao chimbuko lake ni siasa za undumakuwili za nchi za Magharibi na malengo yao maovu katika eneo. 

Mfano wa raia wa Syria ambao wamekuwa wakimbizi kutokana na mgogoro wa vita nchini mwao