Angola yailaumu Ureno, yasema hukumu dhidi ya Makamu wa Rais ni hujuma
Serikali ya Angola imetangaza kuwa, uamuzi wa serikali ya Ureno wa kumtuhumu Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Manuel Domingos Vicente kuwa ametoa rushwa na kutakatisha fedha chafu ni "hujuma nzito" na kwamba inatishia uhusiano kati ya nchi mbili.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola imesema kuwa, Luanda inaitambua njia iliyotumiwa na taasisi za Ureno kutangaza habari hiyo kuwa si za kirafiki na ni hujuma kali dhidi ya Jamhuri ya Angola ambayo inaweza kuvuruga uhusiano mwema wa nchi hizo mbili.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya Ofisi ya Mwendasha Mashtaka Mkuu wa serikali ya Ireno mjini Lisbon kutangaza kuwa, Makamu wa Rais wa Angola, Manuel Vicente anakabiliwa na tuhuma za kutoa rushwa kwa mmoja wa majaji wa nchi hiyo wakati alipokuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya mafuta ya Sonangol.
Manuel Vicente anatambuliwa kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika nchi ya Angola ambayo ndiyo ya pili kwa kuzalisha mafuta ghafi kwa wingi barani Afrika.
Makundi ya kutetea haki za binadamu na taasisi za fedha kama Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) zimeeleza wasiwasi wao kuhusu ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma katika nchi ya Angola ambayo asilimia kubwa ya watu wake wanaishi katika umaskini licha ya utajiri wake mkubwa wa mafuta.