UN yaitaka Guinea-Bissau kuheshimu sheria
Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umewataka viongozi wa kisiasa nchini Guinea-Bissau kuheshimu sheria.
Ujumbe huo uliowasili nchini humo hapo jana kwa ajili ya kuchunguza hali ya mambo, umeyasema hayo wakati wa mazungumzo na Rais wa Guinea-Bissau, José Mário Vaz, Spika wa Bunge na viongozi wa vyama vya kisiasa. Ujumbe huo unaoongozwa na Ismael Martins, balozi wa Angola katika Umoja wa Mataifa umewataka viongozi wa nchi hiyo kuheshimu sheria na kanuni za kidemokra kwa maslahi ya nchi yao. Itafahamika kuwa, Guinea Bissau ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa tangu mwezi Agosti mwaka jana, kufuatia hatua ya Rais Vaz kumpiga kalamu nyekundi waziri wake mkuu Domingos Simoes Pereira. Kufutwa kazi shakhsia huyo kuliifanya nchi hiyo kukosa waziri mkuu kwa miezi kadhaa sasa. Mgogoro wa kisiasa nchini Guinea Bissau umekuwa mkubwa kiasi cha kufanya upatanishi wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (CEDEAO) na Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kireno (CPLP) kushindwa kumaliza mivutano hiyo ya kisiasa.