Apr 13, 2017 07:20 UTC
  • Nchi za mashariki mwa Afrika zaunda kikosi cha pamoja cha kijeshi

Nchi 10 za mashariki mwa Afrika zimeunda kikosi cha pamoja cha kijeshi kitakachofahamika kama East Africa Standby Force (EASF).

Hafla ya kuzindua rasmi kikosi hicho ilifanyika jana katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Kenya KDF, Samson Mwathethe amesema kikosi hicho cha kieneo kinazijumuisha nchi za Kenya, Burundi, Visiwa vya Comoro, Djibouti, Ethiopia, Rwanda, Ushelisheli, Somalia, Sudan na Uganda.

Amesema nchi wanachama wa kikosi hicho cha kieneo (EASF) kadhalika zimezindua Mfuko wa Amani ambao una hazina ya takriban dola milioni moja za Marekani zitakazotumika katika operesheni zake za kijeshi.

Kikosi hicho cha kikanda kimeanza kazi rasmi kujiunga na vikosi vingine vinne vya kieneo vilioundwa na jumuiya za kiuchumi za Ecowas, Eccas, Sadc na Narc.

Askari wa AMISOM nchini Somalia

Sekritariati ya EASF iko katika mtaa wa Karen jijini Nairobi, Kenya huku makao makuu ya kilojistiki ya kikosi hicho cha kieneo yakiwa katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Kikosi hiki kwa sasa kina wanajeshi wake wanaofanya kazi chini ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Somalia AMISOM na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS. 

Azma ya kuwa na kikosi kimoja cha kijeshi barani Afrika ilizaliwa mwaka 2002, katika mkutano wa Umoja wa Afrika, mjini Durban nchini Afrika Kusini, kwa shabaha ya kukomesha utegemezi wa vikosi kutoka nje ya bara hilo.

 

Tags