Polisi wawafyatulia risasi Wanigeria walioandamana kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru
Askari polisi wa Nigeria wametumia risasi moto kuwatawanya waandamanaji wanaotaka kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo (IMN) Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.
Vyombo vya habari vimeripoti kutoka jimbo la Kaduna kuwa maandamano ya amani yaliyofanyika jana ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru yaligeuka ya fujo baada ya polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji.
Maandamano hayo ya jana ya upinzani yamefanyika huku wananchi wa kaskazini mwa Nigeria yaliko makao makuu ya harakati hiyo ya Kiislamu wakiendelea kufanya maandamano ya amani kutaka kiongozi huyo wa kidini aachiliwe huru kama ilivyoamriwa na mahakama.
Ripoti zinaeleza kuwa mamia ya maelfu ya wanachama na wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walishiriki maandamano ya amani yaliyofanyika katika miji kadhaa ikiwemo Katsina, Bauchi, Gombe, Minna na maeneo mengine hapo jana kusisitiza Sheikh Zakzaky aachiliwe huru mara moja.
Mashuhuda wameeleza kwamba kulikuwa na kundi la "wahuni" waliokuwa wakiwasaidia polisi katika kuwakandamiza waandamanaji katika jimbo la Kaduna.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, watu walikuwa wakiandamana kwa amani katika barabara kuu kabla ya polisi na wasaidizi wao kuwafyatulia risasi walipofika kwenye makutano ya Bakinruwa. Mwanamke mmoja alijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini, hatua iliyopelekea waandaaji kuhatimisha maandamano hayo ili kuepusha maafa zaidi.
Viongozi wa IMN wamesema, katika kipindi cha miezi kadhaa nyuma polisi imekuwa ikitoa mafunzo kwa magenge ya wahalifu ili yawashambulie wafuasi wa harakati hiyo ya Kiislamu.
Sheikh Ibrahim Zakzaky alitiwa nguvuni yeye pamoja na mkewe zaidi ya mwaka mmoja uliopita wakati jeshi lilipovamia na kushambulia mkusanyiko wa amani wa kidini wa wanachama wa IMN katika mji wa Zaria kaskazini mwa Nigeria ambapo mamia ya wanachama wa harakati hiyo ya Kiislamu waliuawa…/